August 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubunifu mwanafunzi UDOM kusaidia Walimu kazini



Na Joyce Kasiki, Tanga


MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dickson Chaula, ameibua ubunifu wa mfumo unaolenga kurahisisha shughuli za walimu pamoja na kuwasaidia wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kazi na ofisini.


Chaula amesema ubunifu huo unalenga kutumia teknolojia kutatua changamoto zinazowakabili watumiaji katika mazingira ya kazi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ubunifu unaofanywa na vijana nchini.


Amesema serikali inapaswa kuendelea kutoa msaada kwa wabunifu na wamiliki wa kampuni changa ili kuhakikisha mawazo yenye tija yanageuka kuwa miradi endelevu yenye manufaa kwa jamii.


“Serikali inapaswa kuendelea kutuunga mkono. Tunaona juhudi zinazofanywa, hasa kupitia mpango wa Dira ya Taifa 2050, ikiwamo kupunguza vikwazo vya kodi kwa kampuni changa na kuwezesha upatikanaji wa mikopo na ruzuku kupitia taasisi mbalimbali,” amesema.


Chaula amesema licha ya vijana wengi kuwa na mawazo na ubunifu mzuri, baadhi hushindwa kuendeleza miradi yao kutokana na changamoto za mtaji, ukosefu wa ushauri na kukosa watu wa kuwaongoza katika hatua za awali za uendeshaji wa biashara.


Amesema upatikanaji wa fedha pekee hauwezi kuwa suluhisho la changamoto hizo, kwa kuwa wabunifu wanahitaji pia elimu ya usimamizi wa fedha na uendeshaji wa miradi ili kuhakikisha mitaji inayotolewa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


“Unaweza kumpa mtu mtaji au mkopo, lakini akakosa uelewa wa namna ya kuutumia na kusimamia fedha hizo. Mwishowe anaweza kuzitumia vibaya na ubunifu au biashara yake ikafa,” amesema.


Amesisitiza kuwa serikali na taasisi zinazosaidia wabunifu zinapaswa kuweka mifumo ya ufuatiliaji na ushauri wa kitaalamu ili miradi inayopata msaada iweze kukua na kudumu.


Kwa mujibu wa Chaula, hatua hiyo itasaidia kuongeza uwezekano wa ubunifu wa vijana kuendelea kuwa miradi endelevu, badala ya kuishia katika hatua za mwanzo kutokana na ukosefu wa mtaji, usimamizi na mwongozo.


Amesema kuimarishwa kwa mazingira ya ubunifu kutawapa vijana nafasi kubwa zaidi ya kutumia maarifa na teknolojia kutatua changamoto zilizopo katika jamii na maeneo ya kazi.