Na Mwandishi wetu,Timesmajira
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewataka wataalamu katika taasisi za serikali kuwa wazalendo na kuhakikisha maslahi ya wananchi yanawekwa mbele, hasa katika udhibiti wa dawa na vifaa tiba vinavyoingia nchini.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona dawa au vifaa tiba visivyokuwa na ubora vikiingia nchini kwa msaada wa baadhi ya watu wanaopaswa kulinda afya za Watanzania.
RC Sendiga amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha wahariri wa habari Kanda ya Kaskazini na Mamlaka ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi (TMDA), kilichofanyika Agosti 20, 2026, mkoani Manyara
Aidha, amezitaka taasisi za Serikali nchini kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yao, akisema uelewa wa jamii ni silaha muhimu katika kupata ushirikiano na kulinda maslahi ya Watanzania.

Amesema jamii inapofahamu taasisi inafanya nini, kwa nini inafanya na umuhimu wa huduma zake, huwa rahisi wananchi kuwa sehemu ya kulinda na kuboresha huduma hizo.
Aidha ameipongeza TMDA kwa kuwa mstari wa mbele kulinda afya za jamii tangu kuanzishwa kwake na kusema mkutano huo ni hatua muhimu ya kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi.

“TMDA imeonesha dhamira ya kweli kuhabarisha umma kuhusu dawa na vifaa tiba. Mkutano huu na Wahariri ni mustakabali sahihi na naamini mkitoka hapa mtaenda kutoa taarifa sahihi kwa jamii,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo wa TMDA, Dkt. Yona Mwalwisi aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu Dkt. Adam Fimbo, amesema mamlaka hiyo inaendelea kushikilia cheti cha ISO 9001:2015 na ithibati ya maabara ISO 17025:2017, uthibitisho wa ubora wa huduma zake.

More Stories
Ubunifu wawekwa mbele katika mpango mpya wa Taifa
Ubunifu mwanafunzi UDOM kusaidia Walimu kazini
Teknolojia yarahisisha uendeshaji wa biashara ndogo