Na Joyce Kasiki, Tanga
MWANAFUNZI wa mwaka wa nne wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kelvin Erasto, amebuni mfumo unaolenga kurahisisha mchakato wa watu kununua nguo bila kulazimika kwenda madukani.
Erasto, anayesomea Uhandisi wa Kompyuta na Teknolojia ya Habari, amesema mfumo huo unawawezesha watumiaji kuona na kuchagua nguo kutoka maduka mbalimbali wakiwa nyumbani.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la chuo hicho katika maonyesho ya wiki ya Kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga,mwanafunzi huyo amesema mfumo huo umeunganishwa na maduka tofauti, hivyo mtumiaji anaweza kupata bidhaa zao kupitia mfumo huo na kufanya mchakato wa ununuzi kwa urahisi zaidi.
Erasto amesema bado wanaendelea kurekebisha mapungufu yaliyopo kulingana na maoni ya wateja ambao wameanza kutumia ili kuboresha huduma na kuongeza urahisi kwa watumiaji.
Amesema lengo jingine ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wanaokabiliwa na changamoto katika biashara ya mavazi kukua na baadaye kuwa kampuni kubwa zinazoweza kuuza bidhaa nje ya Tanzania.

More Stories
Maafisa Biashara watakiwa kulinda soko la walaji
PSSSF yawajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya Hifadhi ya Jamii
Prof.Mbarawa:Ukarabati wa Kiwanja cha Ndege Kigoma wafikia asilimia 67