August 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Premier Bet yaendelea kudhamini ligi ya mpira wa Kikapu Dodoma

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

KAMPUNI ya Premier Bet imeingia mwaka wa pili wa ushirikiano na Dodoma Regional Basketball Association (DORBA) katika udhamini wa Dodoma Premier Bet Basketball League, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendeleza vipaji, kuwawezesha vijana na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia michezo.

Akizungumza katika hafla hiyo juzi Mkoani Dodoma,Meneja Masoko wa Premier Bet, Sechelela Kusila, alisema udhamini wa ligi hiyo hauhusiani na kuweka jina la kampuni kwenye mashindano pekee, bali ni sehemu ya dhamira ya muda mrefu ya kampuni katika kuendeleza michezo na vijana nchini.

Amesema safari ya Premier Bet katika kuunga mkono maendeleo ya mpira wa kikapu ilianza mwaka 2022 eneo la Kigamboni Machava, Dar es Salaam, ambapo kampuni ilijenga Premier Projects Arena pamoja na Basketball Academy.

“Tangu hapo, tumeendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo. Mwezi Mei 2025 tulikarabati Vijana Basketball Court, Zanaki, na mwezi Agosti 2025 tukakarabati Mgulani JKT Basketball Court. Pia tunaendelea kusaidia timu za mpira wa kikapu Kigamboni,”amesema Kusila.

Amesema mwaka 2025 kampuni ilipanua dhamira hiyo hadi Dodoma kupitia ushirikiano na DORBA pamoja na udhamini wa Dodoma Spurs Basketball Club, hatua ambayo imeendelea kwa mwaka wa pili.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa DORBA, Godfrey Kishobela, ameishukuru Premier Bet kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu katika kukuza na kuendeleza mpira wa kikapu mkoani Dodoma.

Kishobela amesema ushirikiano huo unatoa fursa kwa wachezaji, makocha na wadau wengine wa mpira wa kikapu kuendeleza vipaji na kuongeza ushindani katika mashindano ya ndani.

Naye Katibu Mkuu wa Tanzania Basketball Federation (TBF), Mwenze Kabinda, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na wadau wa michezo katika kuhakikisha vipaji vya vijana vinapata mazingira bora ya kukua.

Amesema uwekezaji katika michezo ni muhimu kwa sababu unasaidia kujenga nidhamu, mshikamano, kujiamini na kuwapa vijana fursa ya kutumia vipaji vyao kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Meneja wa Premier Bet Mkoa wa Dodoma, Eliatosha Bennedict, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa michezo kuhakikisha mashindano yanaendelea kuwa jukwaa la kuibua na kukuza vipaji vya vijana.

Premier Bet imeeleza kuwa inatarajia msimu wa mwaka huu kuwa na ushindani mkubwa, huku ikiendelea kushirikiana na DORBA, timu, wachezaji, makocha na mashabiki katika kuimarisha maendeleo ya mpira wa kikapu Dodoma.

Udhamini huo unaendelea kuonyesha nafasi ya sekta binafsi katika kusaidia michezo nchini, hususan katika kujenga mazingira yanayowawezesha vijana kukuza vipaji na kushiriki katika shughuli zinazochangia maendeleo ya jamii.