August 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanafunzi abuni Lishe Bora kupambana na utapiamlo

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anayesomea Sayansi ya Chakula na Teknolojia, Fredrick Joseph, ametumia Maonesho ya Nanenane kutambulisha bidhaa ya lishe aliyoibuni kwa kutumia mbegu za mchicha, akilenga kuchangia mapambano dhidi ya utapiamlo na kuhamasisha matumizi ya mazao yenye thamani kubwa ya lishe.


Fredrick amesema bidhaa hiyo imetengenezwa kwa kutumia mbegu za mchicha kama kiungo kikuu, huku ikichanganywa na mbegu za maboga, mtama mweupe na viazi kwa lengo la kuongeza virutubisho muhimu vinavyohitajika mwilini.


Ameeleza kuwa mbegu za mchicha zina kiwango cha protini kati ya asilimia 14 hadi 17 na zina amino asidi muhimu ambazo hazipatikani kwa wingi katika nafaka zinazotumika mara kwa mara kama mahindi na ulezi.


Kwa mujibu wa Fredrick, mbegu hizo pia zina madini ya chuma yanayosaidia kupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa watoto wenye anemia, pamoja na madini ya calcium na magnesium ambayo huchangia kuimarisha mifupa kwa watoto na watu wazima.


Ameongeza kuwa viazi vilivyoongezwa kwenye bidhaa hiyo vina vitamini A inayosaidia kuboresha afya ya macho, huku mbegu za maboga zikitoa protini na mafuta yenye afya yanayomwezesha mtoto kupata nguvu na kukua vizuri.


Fredrick amesema lengo la kushiriki Maonesho ya Nanenane ni kuitambulisha jamii bidhaa hiyo pamoja na kuhamasisha matumizi ya mazao ambayo mara nyingi hupuuzwa, licha ya kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha lishe na afya.
Amesema matumizi ya mazao hayo yanaweza kuwa sehemu ya suluhisho la kupunguza utapiamlo na kuboresha afya ya jamii kwa ujumla.