July 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwalimu auawa akizuia mifugo kupitia eneo la shule

Na Moses Ng’wat, Songwe.

MWALIM wa Shule ya Sekondari Galula, wilayani Songwe, Nisetas Dimoso, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa wafugaji alipowazuia kupitisha mifugo ndani ya eneo la shule.

Mwalimu huyo alifariki dunia 28, 2026, akiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya alikokuwa akipatiwa matibabu ya majeraha anayodaiwa kuyapata katika shambulio lililotokea usiku wa saa mbili ya Julai 26, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, inadaiwa kuwa, tukio lilianza baada ya vijana wawili kujaribu kupitisha mifugo katikati ya eneo la Shule ya Sekondari Galula, ambapo
Mwalimu Dimoso, hatua inayodaiwa kuzua mabishano na kuzusha ugomvi.

Inadaiwa mmoja wa vijana hao aliwapa taarifa watu wengine wanaodaiwa kuwa wamiliki wa mifugo waliokuwa jirani, ambao walifika eneo hilo na kumshambulia mwalimu huyo kwa kipigo kabla ya kutoweka.

Walimu na wananchi walimkimbiza Mwalimu Dimoso katika Kituo cha Afya Mbuyuni Wilayani humo kwa huduma ya kwanza, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, ambako alifariki dunia akiwa anaendelea na matibabu.

Diwani wa Kata ya Galula, Mikozi Mwavilundo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema lihusisha watu wanaodaiwa kutoka katika familia ya mtu aliyetambulika (jina limehifadhiwa).

Mwavilundo amesema licha ya taarifa kutolewa mapema katika Kituo Kidogo cha Polisi Galula na watuhumiwa wanaodaiwa kufahamika, hadi sasa hakuna aliyekuwa amekamatwa, jambo lililozua hofu na maswali miongoni mwa wananchi.

Diwani huyo, ameongeza kuwa tukio ni la pili kwa mtumishi kushambuliwa katika eneo hilo, kwani mwezi wa tatu mwaka huu, mtendaji wa kitongoji katika kijiji hicho alishambuliwa na wafugaji na kupoteza maisha.