Na Mwandishi Maalumu,Timesmajira
Wananchi wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima saratani mara kwa mara ili kama watagundulika kuwa na ugonjwa huo waweze kupata matibabu mapema kwani saratani ikigundulika mapema inatibika.
Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu ya saratani zinazotolewa na taasisi hiyo pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali.
Dkt. Msemo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani alisema ugonjwa huo kama yalivyo magonjwa mengine unatibika iwapo utabainika katika hatua za awali na mgonjwa kupata matibabu sahihi kwa wakati.
“Matibabu ya Saratani ni tofauti na matibabu ya magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza, iwapo mgonjwa atabainika mapema kuwa na tatizo atatibiwa na kupona na kuendelea na maisha yake ya kawaida bila ya kutumia dawa”, amesema Dkt. Msemo.
Amesema zipo aina mbalimbali za Saratani, ikiwemo Saratani ya tezi dume na kuwataka wanaume wenye umri wa miaka 45 na kuendelea kujitokeza kupima ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Dkt. Msemo baadhi ya wanaume huogopa kupima Saratani ya tezi dume kutokana na imani potofu kuwa uchunguzi wake hufanywa kwa njia isiyo rafiki.
Amesema uchunguzi wa awali unaweza kufanyika kwa urahisi kama vile kupima maralia na iwapo kutabainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo, mgonjwa atafanyiwa vipimo vingine vikiwemo vya ultrasound au CT scan kulingana na ushauri wa daktari.
“Kila mwanaume ana tezi dume ambayo ipo karibu na njia ya mkojo. Dalili kama kukojoa kwa shida zinaweza kuashiria uwepo wa uvimbe unaozuia mkojo kupita. Hata hivyo uvimbe huo si lazima uwe wa saratani ndiyo maana uchunguzi wa mapema ni muhimu kufanyika”, amesema Dkt. Msemo.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya saratani amesema baadhi ya wagonjwa huchelewa kufika hospitalini kupata matibabu kwa kutegemea tiba mbadala hii ni kutokana na imani potofu waliyonayo kuhusu matibabu ya Saratani.
Amesema kuchelewa huko kunawafanya baadhi ya wagonjwa kufika hospitalini wakiwa katika hatua za tatu au nne za ugonjwa hali inayoweza kufanya matibabu kuwa magumu zaidi.
Dkt. Msemo amesema ORCI inaendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na huduma za uchunguzi wa Saratani kwa kufanya kambi mbalimbali za uchunguzi wa ugonjwa huo. Aliwashukuru waandishi wa habari kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo.

More Stories
Mabasi ya umeme Zanzibar kutumia malipo kidijitali
GGML kuimarisha ushiriki wa watanzania sekta ya madini
Elimu usalama barabarani yatolewa kwa askari wa JWTZ