July 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sangu: Tanzania kushiriki maonesho ya 26 ya Wajasiliamali Kigali

Na Israel Mwaisaka, Rukwa

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu – kazi ,ajira na mahusiano Deus Sangu amesema Tanzania itashiriki maonesho ya 26 ya wajasiriamali wadogowadogo,wadogo na wa kati(MSMEs)ya jumuiya ya afrika mashariki maarufu kama nguvu kazi/ jua kali yatakayofanyika Jijini Kigali – Rwanda kuanzia 30 oktoba ,2026 hadi 8 Novemba ,2026.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Julai 23 ,2026 katika ukumbi wa NSSF manispaa ya Sumbawanga Sangu amesema wajasiriamali wapatao 1,000 kutoka nchi 8 wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki watashiriki maonesho hayo.

Amesema Tanzania itawakilishwa na wajasiriamali 250, na serikali itawagharamia kwa kuwasafirisha wao na bidhaa zao.

Ameongeza kuwa lengo la maonesho hayo yanayotambuliwa kama maonesho ya nguvu kazi/jua kali yanalenga kuwainua wajasiriamali wadogowadogo, wadogo na wa kati waliopo katika sekta isiyo rasmi.

“Maonesho haya yanalenga kuwawezesha wajasiriamali kurasimisha shughuli zao kwa kuwapatia fursa ya kutangaza bidhaa ,kubadilishana taarifa na uzoefu ,kukuza ujuzi ,kukuza masoko ya bidhaa na teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa na hatinaye kuongeza fursa za ajira za staha kwa watanzania.”amesema Sangu.

Ameongeza kuwa maonesho hayo yalifanyika mara ya kwanza mwezi Desemba ,1999 Jijini Arusha – Tanzania sambamba na sherehe za utiaji Saini wa mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya ya afrika mashariki uliofanyika tarehe 30,Novemba ,1999 zikiwepo nchi za Kenya ,Uganda, na Tanzania na kuhudhuriwa na wakuu wa Nchi wanachama.