Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar Es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu,Prof. Palamagamba Kabudi amepongeza watendaji wa Manispaa ya Ubungo kwa ubunifu wa ununuzi wa mitambo ya kutengeneza barabara itakayosaidia mageuzi ya uimarishaji wa mtandao wa barabara na kuchochea shughuli za maendeleo na kasi ya ukuaji wa uchumi kwa wananchi.
Prof. Kabudi ameitoa pongezi hizo leo tarehe 20 Julai, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati aliposhiriki katika uzinduzi wa mitambo ya malori ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo itakayosaidia katika kuboresha miundombinu ya bararaba katika halmashauri hiyo.

“Maamuzi haya si mepesi kufanywa na baraza la madiwani, kwa sababu imelenga kutatua changamoto za barabara zinazotukabili kwa sasa, ni lazima mitambo hii isimamiwe sawasawa ili kuleta tija kwa wananchi na kila mtendaji aone anajukumu la kuilinda mitambo hii” ameeleza Prof. Kabudi
Aidha, Prof. Kabudi amesema, “ubunifu wa namna hii unahitajika sana, kufanywa katika maeneo mengine ili Halmashauri kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA) na kwa kutumia nyenzo uwe wa faida kwa wananchi na mambo haya yanawekewa mkazo kwenye dira ya Taifa.”
Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amesema malengo ya Mkoa wake ni kutoka kwenye kuwaza mambo madogo na kuwaza mambo makubwa yenye tija kwa taifa.

“Ili kufikia matarajio hayo tumeainisha kwamba maendeleo lazima yawe yanahusu watu, maendeleo yanayoweza kuchangiwa na watu na yawe maendeleo yao wenyewe,” ameeleza Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Albert Msando amesema, msukumo wa kununua mitambo hiyo ulitokana na kulenga kukarabati barabara zinazoharibika wakati wa masika na hasa barabara za mtaani ambazo ziko katika utaratibu wa kusajiliwa na Wakala wa Barabara vijijini na Mjini (TARURA).
“Imani yetu kwa ngazi ya wilaya ni kuendelea kuwekeza zaidi kwa kujipanga kununua seti nyingine ya mitambo ili kusaidia kila jimbo kuwa na mitambo yake ili kupata matokeo mazuri,” alifafanua Msando.



More Stories
Sangu atoa onyo matumizi mabaya fedha za miradi
Mpango wa Serikali wa uanangezi wawanufaisha halmashauri Sumbawanga
UNDP yanoa watengeneza maudhui Songwe