Na Mwandishi Wetu,
RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),ambaye pia ni Kansela wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT), na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa, amemteua Padri Profesa Emmanuel Wabanhu kuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho kuanzia Agosti 1, 2026.
Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Ibara ya 11 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 10 ya Hati ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania ya mwaka 2012, iliyochapishwa kupitia Tangazo la Serikali Na.580 la mwaka 2020 chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu,Sura ya 346,toleo lililofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Prof. Wabanhu ni Padri wa Jimbo Katoliki la Geita na Profesa Mshiriki mwenye uzoefu katika taaluma ya teolojia ya maadili, akibobea katika maadili tetezi (applied ethics).
Amekuwa mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA),Nairobi nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 13,kabla ya kuhudumu kwa miaka miwili kama Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utawala na Fedha katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mihayo cha Tabora (AMUCTA).
Mbali na uzoefu wake wa kitaaluma, Prof.Wabanhu ameandika vitabu vitano na kuchapisha zaidi ya makala 20 za kitaaluma katika majarida yanayotambuliwa kimataifa.
Kitaaluma,anashikilia Shahada ya Kwanza ya Teolojia kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana,Roma nchini Italia,Shahada za Uzamili katika Masomo ya Dini na Teolojia,Shahada ya Uzamivu wa Teolojia Takatifu (STD), pamoja na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Maadili ya Jamii na Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Katholieke Universiteit Leuven nchini Ubelgiji.
Katika taarifa iliyotolewa Julai 15,2026 na Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya SAUT imempongeza Prof.Wabanhu kwa uteuzi huo na kueleza imani kuwa atalitekeleza vyema jukumu lake jipya.
Hata hivyo chuo hicho pia kimewataka wanajamii wa SAUT na wadau wote kumpa ushirikiano na msaada anapoanza majukumu yake mapya.

More Stories
Mradi wa maji wanufaisha wakazi 22,000
Shule 10 kunufaika na mpango wa kuboresha ufaulu
Future World,Chanika Veteran hakuna mbabe mechi ya Kirafiki