July 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa maji wanufaisha wakazi 22,000

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.

Kupitia mradi wa kuboresha mfumo wa usambazaji maji katika Mji wa Misungwi mkoani Mwanza,zaidi ya wakazi 22,000 wameanza kunufaika na maboresho yaliofanyika kupitia mradi huo kwa kupata huduma ya maji safi.

Hayo yamebainishwa leo kupitia taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha MWAUWASA,ambapo taarifa hiyo imesema kuwa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 880 umefikia asilimia 98 ya utekelezaji.

Mradi huo umehusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji,choteo la maji lenye ukubwa wa lita za ujazo 50,000,matenki mawili yenye ujazo wa lita 150,000 na 90,000.

Pia ununuzi na ufungaji wa pampu mbili za kusukuma maji zenye uwezo wa kuzalisha lita 50,000 kwa saa,ununuzi na ufungaji wa “transformer KV” 100, ununuzi na ulazaji wa mabomba yenye ukubwa wa mm 160 na 110 aina ya “HDPE PN 16” kwa umbali wa km 3.5, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 10 na ujenzi wa chemba 10 za kuhifadhi “valves”.

Huku kukamilika kwake kukiongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Misungwi hadi asilimia 97,ambapo kupitia mradi huo wakazi wapatao 22,482 waishio maeneo ya vijiji vya Ng’ombe, Iteja, Mbela “B”, Mbela “D”, Mbela “C”, Old Misungwi, Mwamanga na Mitindo “B” wameanza kunufaika.

Hata hivyo sehemu ya taarifa hiyo imesema kuwa hatua hiyo ya kuongezeka kwa asilimia za upatikanaji wa maji katika Mji wa Misungwi itasaidia kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Sanjari na hayo mradi huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Agosti 16,2026 na Mwenge wa Uhuru.