Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga
SHULE 10 za sekondari jijini Tanga ambazo zimekuwa na matokeo duni katika mitihani ya Taifa kwa kipindi cha miaka mitatu hadi minne mfululizo, zimeingizwa katika mpango maalum wa kuboresha ufaulu.
Mpango huo unaolenga kuongeza kiwango cha mafanikio ya wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne pamoja na kubaini chanzo halisi cha changamoto zinazochangia matokeo hayo huku shule ziluzonufaika ni Nguvumali, Mikanjuni, Hoteni, Kihere, Mwapachu, Tongoni, Kirare, Marungu, Mabokweni pamoja na shule nyingine iliyochaguliwa chini ya tathmini ya mradi huo.

Mpango huo unatekelezwa na TangaYetu kwa ufadhili wa Botnar Foundation ya Uswisi kwa kushirikiana na taasisi ya Innovex na Tanzania Centre for Education, ukiwa na lengo la kuinua ubora wa elimu katika Jiji la Tanga kupitia mafunzo kwa wanafunzi,walimu na wadau wa elimu.
Akizungumza jana wakati wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mwapachu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Centre for Education,Yusuph Ugutu alisema, shule hizo zilichaguliwa baada ya tathmini kubaini kuwa zimekuwa zikifanya vibaya katika mitihani ya taifa kwa miaka mitatu hadi minne mfululizo.
Amesema programu hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kujifunza mbinu za kujibu maswali ya mitihani na kuongeza ari ya kufanya vizuri, huku ikitoa fursa ya kubaini changamoto zinazokwamisha ufaulu.
Pia amesema mpango huo utahusisha walimu, Maofisa Elimu wa Kata na  Halmashauri ya Jiji la Tanga pamoja na wadau wengine wa elimu kupitia semina mbalimbali zitakazolenga kuboresha mbinu za ufundishaji na usimamizi wa elimu.
Kwa mujibu wa Ugutu, alisema tathmini ya matokeo ya shule hizo imeonesha kuwa baadhi zimekuwa zikikosa wanafunzi wanaopata daraja la kwanza, huku idadi ya wanaofaulu kwa daraja la pili ikiwa ndogo, hali iliyoifanya taasisi hiyo kuanzisha programu maalum ya kuokoa kiwango cha ufaulu.
Kwa upande wake,Ofisa Elimu wa Kata ya Masiwani,Mohamed Matumbo amesema,mpango huo umekuja wakati muafaka kwani utawasaidia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na kidato cha nne kuwa na maandalizi bora zaidi.
Amesema wanafunzi wengi hukumbwa na changamoto za lugha,uelewa wa maswali pamoja na mbinu za kujibu mitihani,hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza kujiamini na kufanya vizuri.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa programu hiyo imewapa matumaini mapya ya kuboresha matokeo yao, wakisema wamepata mbinu bora za kujifunza, kupanga muda wa masomo na kujibu maswali ya mitihani kwa ufanisi.
Wamesema pia mafunzo yatakayotolewa kwa walimu yataongeza ubora wa ufundishaji darasani, jambo litakalosaidia kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika shule zao.

k

More Stories
Profesa Wabanhu ateuliwa kuwa Makamu Mkuu SAUT
Mradi wa maji wanufaisha wakazi 22,000
Future World,Chanika Veteran hakuna mbabe mechi ya Kirafiki