July 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndoto zilizovunjika: Jinsi Mimba za utotoni zinavyowakatisha Wasichana elimu nchini Rwanda,Tanzania na Sudan Kusini

Na.Waandishi wetu

KATIKA nchi za Afrika Mashariki, maelfu ya wasichana wanaendelea kupoteza haki yao ya elimu kutokana na mimba za utotoni licha ya kuwepo kwa sera na miongozo inayolenga kuwawezesha kuendelea na masomo yao.

Takwimu za hivi karibuni za Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu nchini Rwanda zinaonesha kuwa kiwango cha mimba za utotoni kimeongezeka kutoka asilimia 5 mwaka 2019/20 hadi asilimia 8 mwaka 2025.

Nchini Tanzania, zaidi ya wasichana 30,000 wamepata nafasi ya kurejea shuleni kupitia sera ya kurejea masomoni baada ya kujifungua. Wakati huo huo, nchini Sudan Kusini, inakadiriwa kuwa asilimia 30 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 hupata ujauzito, huku ndoa za utotoni zikiendelea kuwa changamoto kubwa.

Mahojiano yaliyofanywa katika nchi hizi tatu yanaonesha kuwa mimba, unyanyapaa, umaskini na kukataliwa na familia ndiyo sababu kuu zinazowakatisha wasichana wengi safari yao ya elimu.

Rwanda: Mimba, Unyanyapaa na Mwisho wa Safari ya Elimu

Eugenie Iradukunda alikuwa na umri wa miaka 13 tu alipogundua kuwa alikuwa mjamzito. Wakati huo alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa sekondari akiwa na ndoto za kumaliza masomo yake.

Kabla hajapata nafasi ya kumweleza mtu yeyote kuhusu ujauzito wake, mama yake alikuwa tayari ameshagundua. Badala ya kupata faraja nyumbani, Eugenie alikumbana na kukataliwa.

“Mama yangu aliniambia kuwa hangeweza kuvumilia aibu niliyokuwa nimeiletea familia na hata akasema angejiua,” anakumbuka.

“Niliogopa sana na kuamua kukimbia nyumbani. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa maisha yangu nje ya shule.”

Baada ya kujifungua, Eugenie alitarajia kuruhusiwa kurejea shuleni. Hata hivyo, wazazi wake walimweleza kuwa hawakuwa na uwezo wa kugharamia elimu yake pamoja na mahitaji ya mtoto wake.

Kisa chake kinafanana na cha Sandrine Umuhoza, ambaye sasa ni mama wa mtoto mwenye umri wa miezi mitatu.

Sandrine alipata ujauzito akiwa bado mwanafunzi wa darasa la nne la shule ya msingi. Muda mfupi baadaye, mama aliyekuwa akiishi naye alifariki dunia na kumuacha chini ya malezi ya bibi yake.

“Bibi yangu alinishauri niache shule kwa sababu hakuwa na uwezo wa kunihudumia mimi na mtoto wangu kwa wakati mmoja,” anasema Sandrine.

“Bado nina matumaini ya kurejea shuleni siku moja, lakini ni baada ya mtoto wangu kukua. Kwa sasa hilo haliwezekani.”

Kwa Joyce Niyigena, ujauzito haukusababisha tu kuacha shule bali pia kupoteza makazi.

Joyce alipata ujauzito akiwa darasa la sita. Familia yake ilipogundua hali hiyo, ilimfukuza nyumbani mara moja.

“Walihisi nimeiletea familia aibu kubwa,” anasema.

“Niliishi mitaani na huko ndiko nilikojifungulia. Wafanyakazi wa afya waliwasiliana na familia yangu lakini walikataa kunipokea tena. Leo hii sina makazi na kurejea shuleni ni jambo ambalo siwezi hata kulifikiria.”

Ingawa simulizi zao zinatofautiana, zinaonesha hali halisi inayowakumba wasichana wengi nchini Rwanda. Kwa wengi wao, ujauzito huwa mwanzo wa mwisho wa safari ya elimu.

Kukataliwa na familia, umaskini, unyanyapaa na jukumu la kulea mtoto hujenga vikwazo vikubwa ambavyo wasichana wengi hushindwa kuvivuka.

Sera Zinatoa Matumaini, Lakini Uhalisia Bado Ni Mgumu

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya nchini Rwanda, zaidi ya vijana 23,000 hupata ujauzito kila mwaka. Ingawa athari za kiafya za mimba za utotoni hupewa kipaumbele mara nyingi, wataalamu wanasema madhara yake ya muda mrefu ni pamoja na kuacha shule, umaskini, ukosefu wa ajira, msongo wa mawazo na kutengwa kijamii.

Serikali ya Rwanda imeanzisha mikakati mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo. Mpango wa Mkakati wa Sekta ya Elimu wa mwaka 2024–2029 unalenga kupunguza wanafunzi wanaoacha shule na kuimarisha njia za kuwarejesha katika mfumo wa elimu watoto na vijana walio nje ya shule. Sera za taifa pia zinawaruhusu wasichana waliopata ujauzito kurejea shuleni baada ya kujifungua.

Hata hivyo, mahojiano yaliyofanywa katika uchunguzi huu yanaonesha kuwa wasichana wengi hawawezi kunufaika na fursa hizo. Umaskini, majukumu ya kulea watoto, unyanyapaa na ukosefu wa msaada kutoka kwa familia vinaendelea kuwazuia wengi wao kurejea darasani.

Mtaalamu wa afya anayejikita katika masuala ya jinsia, Alice Bumanzi, anaamini kuwa mimba nyingi za utotoni zinaweza kuzuilika ikiwa vijana watapata taarifa sahihi mapema.

“Watoto wengi hawajui namna ya kujilinda wanapoanza kupitia mabadiliko ya kimwili na kihisia wakati wa balehe,” anasema.

“Wanahitaji kupata elimu sahihi na inayolingana na umri wao kuhusu afya ya uzazi kabla ya ujauzito kutokea. Bila elimu hiyo, wengi hutambua madhara yake baada ya kuacha shule tayari.”

Maafisa wa Serikali wanakiri kuwa kupunguza mimba za utotoni kunahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali.

Aline Umutoni, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Familia na Ulinzi wa Mtoto katika Wizara ya Jinsia na Ustawi wa Familia nchini Rwanda, anasema wasichana wanaopata ujauzito, hasa kutokana na ukatili wa kingono, hukumbwa na majeraha makubwa ya kihisia yanayochangia kuacha shule.

“Mtoto anayepata ujauzito baada ya kufanyiwa ukatili wa kingono anaweza kupata msongo mkubwa wa mawazo au kuacha shule kabisa. Kukabiliana na changamoto hii kunahitaji ushiriki wa familia, shule, jamii na taasisi zote zinazohusika na ulinzi wa watoto,” anasema.

Naye Waziri wa Afya wa Rwanda, Dkt. Sabin Nsanzimana, anasema kupunguza mimba za utotoni ni jukumu la kila mtu.

“Mimba za utotoni si suala la wasichana pekee. Wengi huacha shule, huku familia zikifanya maamuzi magumu yanayozidisha matatizo yao. Walimu pia wana wajibu kwa sababu mwanafunzi anapopata ujauzito akiwa shuleni, kila mmoja anatakiwa kujiuliza ni nini kingefanyika tofauti. Serikali ya Rwanda imejizatiti kuhakikisha hakuna msichana anayepoteza elimu kwa sababu ya ujauzito kwa kupanua huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana na kuimarisha elimu ya afya ya uzazi mashuleni.”

Tanzania: Nafasi ya Pili ya Elimu, Lakini Safari Bado Ni Ngumu

Nchini Tanzania, sera inayowaruhusu wasichana waliokatisha masomo kutokana na ujauzito kurejea katika mfumo wa elimu imeleta matumaini mapya kwa maelfu ya wasichana.

Tangu miongozo ya kurejea shuleni ilipoanza kutekelezwa mwaka 2021, zaidi ya wasichana 22,844 walikuwa wamerejea katika elimu rasmi na mbadala kufikia Machi 2024. Kati yao, 5,142 walirejea katika shule za kawaida, huku 17,702 wakijiunga na programu za elimu mbadala.

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa idadi hiyo imeongezeka na sasa zaidi ya wasichana 30,000 wamepata fursa ya kuendelea na masomo yao. Hata hivyo, kurejea darasani hakujafuta changamoto zinazowakabili.

Wasichana wanaorejea shule baada ya kujifungua hukumbana na vikwazo vingi vinavyotishia safari yao ya elimu. Unyanyapaa kutoka kwa jamii, wanafunzi wenzao na hata baadhi ya walimu huathiri hali yao ya kujiamini na afya ya akili. Wengine hulazimika kugawanya muda kati ya malezi ya mtoto na masomo, jambo linalopunguza uwezo wao wa kufanya vizuri kitaaluma.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa miundombinu rafiki kwa mama na mtoto katika shule nyingi, ikiwemo maeneo ya kunyonyesha na huduma zinazozingatia mahitaji ya watoto wadogo. Aidha, ugumu wa maisha na ukosefu wa fedha huongeza hatari ya wasichana hao kuacha shule kwa mara nyingine.

Wataalamu wa elimu na haki za watoto wanaonya kuwa kuwapa wasichana nafasi ya kurejea shule pekee haitoshi. Wanasema kuna haja ya kuimarisha huduma za ushauri nasaha, msaada wa kijamii na uwekezaji katika mazingira salama ya kujifunzia.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kati ya asilimia 20 hadi 28 ya wasichana wanaorejea shule baada ya kujifungua hujikuta wakiacha masomo tena kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo.

Licha ya changamoto hizo, takwimu za Serikali zinaonesha kuwa kati ya Januari 2021 na Januari 2022, wanafunzi wa kike 9,011 walipata ujauzito wakiwa shuleni. Kati yao, 1,554 walikuwa wa shule za msingi na 7,457 walikuwa wa shule za sekondari.

Hali hiyo inaonesha ukubwa wa changamoto inayokabili mfumo wa elimu nchini Tanzania na umuhimu wa kuendelea kuimarisha mikakati ya kuwalinda na kuwawezesha wasichana kuendelea na masomo yao hata baada ya kukumbwa na ujauzito.

Unyanyapaa Bado Ni Kikwazo Kikubwa kwa Wasichana Wanaorejea Shuleni

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiative, Consolata Chikoti, anasema licha ya kuwepo kwa sera ya kurejea shuleni, wasichana wengi wanaorudi masomoni baada ya kujifungua bado wanakumbana na unyanyapaa, ubaguzi na kutengwa katika jamii.

Anasema taasisi yake inaendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za kuwalinda wasichana hao, lakini takwimu zinaonesha kuwa wengi bado wanapata ugumu wa kuzoea tena mazingira ya shule.

“Takwimu za Global Women Institute zinaonesha kuwa takribani wasichana milioni 60 duniani wamewahi kukumbwa na ukatili wa kijinsia. Nchini Tanzania, wasichana wapatao milioni 14.6 wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha haki yao ya kupata elimu,” anasema Chikoti.

Anaeleza kuwa kupitia mradi wa Back to School, zaidi ya wasichana 500 tayari wamefikiwa na kupatiwa msaada, huku mwaka 2026 pekee taasisi hiyo ikilenga kuwafikia wasichana wengine 250.

Kwa mujibu wake, unyanyapaa kutoka kwa wanafunzi wenzao, jamii na wakati mwingine walimu, umeendelea kuwa moja ya vikwazo vikubwa vinavyowazuia wasichana wengi kufanikiwa wanaporejea shuleni.

Licha ya changamoto hizo, kuna simulizi nyingi za mafanikio. Baadhi ya wasichana waliorejea shuleni wameendelea kufanya vizuri kitaaluma na wengine wamefanikiwa kuingia katika ngazi za juu za elimu.

Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa hadi Machi 2024, jumla ya wasichana 22,844 waliokuwa wameacha shule kutokana na ujauzito walikuwa wamerejea katika mfumo wa elimu. Kati yao, 5,142 walirejea katika shule za msingi na sekondari, huku 17,702 wakijiunga na programu za elimu mbadala.

Mtaalamu Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Gladness Kirei, anasema kuna umuhimu mkubwa wa wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kuacha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.

Anasema Serikali imebaini kuwa baadhi ya wanafunzi waliorejea chini ya mwongozo wa mwaka 2021 wamekuwa wakiacha shule tena kutokana na unyanyapaa kutoka kwa jamii, walimu na wanafunzi wenzao.

“Kuna wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya ubaguzi na unyanyapaa unaowafanya wajione hawakubaliki. Mwongozo unaeleza wazi kuwa mwanafunzi anayokumbana na hali hiyo katika shule moja ana haki ya kuhamia shule nyingine,” anasema Dkt. Kirei.

Anasisitiza umuhimu wa kuwapatia wanafunzi hao vifaa vya shule, msaada wa kisaikolojia na motisha ili waweze kutimiza ndoto zao.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa tangu kuanza kwa utekelezaji wa sera ya kurejea shuleni mwaka 2021, maelfu ya wasichana waliokatisha masomo kutokana na ujauzito wamepata fursa ya kuendelea na elimu yao.

Kwa mujibu wake, mwaka 2025 pekee, takribani wasichana 10,300 waliopata ujauzito walirejea masomoni katika shule zao za awali au taasisi nyingine za elimu baada ya kujifungua.

“Bado Ninaota Kuwa Mwanasaikolojia”

Miongoni mwa wasichana waliopitia changamoto hizo ni Kuruthum Jumaa (si jina lake halisi), ambaye alilazimika kuacha shule baada ya kupata ujauzito akiwa na umri wa miaka 15.

Kuruthum anasema ndoto yake ilikuwa kuwa mwanasaikolojia ili kusaidia wasichana wanaokumbana na changamoto mbalimbali katika maisha yao.

Anasimulia kuwa alipokuwa akijiandaa kuanza masomo ya sekondari, baba yake alifariki dunia. Katika kipindi hicho kigumu, alijikuta akipata ujauzito kutokana na mazingira magumu ya kifamilia yaliyotokana na msiba huo.

Baada ya kupata ujauzito, alilazimika kuacha shule. Hali ilizidi kuwa ngumu zaidi baada ya mwanaume aliyempa ujauzito kutoweka kwa hofu ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Nikikumbuka bado naumia. Nilikuwa nimefaulu vizuri mtihani wangu wa kuhitimu shule ya msingi na nilikuwa tayari kuanza kidato cha kwanza. Baada ya kupata ujauzito nilifukuzwa nyumbani na nilipitia mateso makubwa,” anasema.

“Nililazimika kujitafutia ada za shule kwa kufanya biashara huku nikimlea mtoto wangu.”

Anasema changamoto kubwa inayomkabili hadi leo ni unyanyapaa.

“Nilipoamua kurejea shuleni, watu wengi, hata baadhi ya ndugu, walinikatisha tamaa. Maneno yao karibu yanifanye niachane kabisa na ndoto yangu.”

Kutokana na hofu ya kuhukumiwa na jamii, Kuruthum anasema hata sasa havai sare ya shule.

“Ninaingia darasani nikiwa nimevaa nguo za kawaida kwa sababu naogopa watu watanihukumu. Mara nyingi nampeleka mtoto wangu shuleni. Wakati wa mapumziko namnyonyesha kisha narudi darasani kuendelea na masomo.”

Licha ya changamoto zote hizo, bado hajakata tamaa.

“Ndoto yangu bado ni kuwa mwanasaikolojia ili niweze kuwasaidia wasichana wengine wanaopitia changamoto kama nilizopitia mimi.”

Sudan Kusini: Wakati Ujauzito Unapofunga Mlango wa Darasa

Juan (si jina lake halisi) ni mmoja wa wasichana hao. Baada ya kukimbia machafuko ya mwaka 2016 yaliyolikumba eneo la Kajo Keji na kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Morobi nchini Uganda, aliamini kuwa maisha yake yangepata mwelekeo mpya aliporejea Juba kuendelea na masomo.

Mjomba wake alimkaribisha mjini humo na kumhimiza arejee shule ili kufidia miaka aliyopoteza akiwa kambini. Kila siku alikuwa akipelekwa shuleni na dereva wa bodaboda ili kuhakikisha anafika kwa wakati.

Hata hivyo, ndoto zake zilianza kufifia alipoanzisha uhusiano wa kimapenzi na dereva huyo ambaye baadaye alimshawishi kufanya ngono, hali iliyosababisha ujauzito usiopangwa.

“Sikujua kama nilikuwa mjamzito hadi nilipoacha kuona siku zangu za hedhi. Nilifikiria kutoa mimba, lakini niliogopa,” anasema huku akibubujikwa na machozi.

Akiwa katika kituo cha afya cha msingi eneo la Gurei, Juan anasema ujauzito huo umeharibu uhusiano wake na wazazi wake ambao sasa wanaamini kuwa amewasaliti.

“Wazazi wangu walipogundua, walikasirika sana na kuniambia niende nikamtafute mume wangu,” anasema.

Ndoto yake ya kuwa muuguzi sasa imebakia kuwa kumbukumbu.

Kisa kingine ni cha Kiden (si jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 16, ambaye anaishi Kajo Keji akiwa na mtoto wa miezi sita aliyemzaa mwaka 2025 akiwa kambini.

Kiden anasema mwanaume aliyempa ujauzito alitoweka mara baada ya tukio hilo, jambo lililomlazimu kurejea kijijini baada ya shangazi yake kumweleza kuwa hakuwa na uwezo wa kuendelea kumlea yeye pamoja na mtoto wake.

“Nilikuwa nimeenda kuchota maji jioni kwenye kisima ndipo nilipokutana na mwanaume aliyenilazimisha kufanya naye ngono. Sikuthubutu kumweleza shangazi yangu kwa sababu niliogopa angenifukuza,” anasimulia.

Kwa sasa anajikimu kwa kufanya kazi za kulima mashambani kwa ujira mdogo ili aweze kumhudumia mtoto wake.

“Nafasi ya kurejea shuleni imekuwa ndoto ambayo sioni kama inaweza kutimia tena,” anasema.

Umaskini, Migogoro na Ndoa za Utotoni

Sudan Kusini inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa ya mimba za utotoni, ambayo imekuwa moja ya sababu kuu za wasichana kuacha shule pamoja na umaskini, migogoro ya kivita, ukosefu wa usawa wa kijinsia na mila kandamizi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wasichana ya Juba One, Clemetina Kiden Arkanjelo, anasema mimba za utotoni bado ni sababu kubwa ya wanafunzi wa kike kuacha shule licha ya sera zinazowaruhusu kurejea masomoni baada ya kujifungua.

Anasema ukosefu wa huduma za malezi ya watoto ni moja ya changamoto kubwa zinazowazuia mama vijana kurejea darasani.

“Wengi hawana mtu wa kuwaangalia watoto wao wanapokuwa shuleni, jambo linalowafanya washindwe kuendelea na masomo,” anasema.

Mradi wa Girls Education South Sudan (GESS), ambao ulikuwa ukitoa msaada wa kifedha kwa wanafunzi wa kike wa shule za msingi, uliwahi kusaidia wasichana wengi kubaki shuleni. Hata hivyo, baada ya mradi huo kusitishwa, familia nyingi maskini zimeendelea kukumbwa na changamoto za kifedha zinazowasukuma watoto wao kuacha shule.

Ingawa Wizara ya Elimu ya Sudan Kusini imeweka sera inayoruhusu wanafunzi wajawazito na mama vijana kuendelea na masomo na kupiga marufuku kufukuzwa shule au kunyimwa mitihani, wadau wanasema bado kuna safari ndefu ya kuhakikisha sera hiyo inatekelezwa kikamilifu.

Wito wa Kulinda Haki ya Wasichana Kupata Elimu

Mwanaharakati wa haki za wanawake na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Women for Justice and Equality, Zabib Musa Loro, anasema mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia vinaendelea kuwanyima maelfu ya wasichana haki yao ya elimu nchini Sudan Kusini.

Anasema tatizo hilo linachochewa na ubakaji, umaskini, migogoro ya kivita na mifumo dhaifu ya ulinzi wa watoto.

Kwa mujibu wake, baadhi ya familia huwalazimisha mabinti zao kuolewa mapema ili kupata fedha au mali, huku migogoro ya kivita ikiongeza hatari ya wasichana kukumbwa na unyonyaji na ukatili wa kijinsia.

Loro pia anaeleza kuwa mazingira ya ukatili wa nyumbani huwafanya baadhi ya wasichana kukimbia makwao na kujikuta katika mazingira hatarishi.

“Haya yote huwafanya wasichana kuacha shule na wakati mwingine kutengwa hata na familia zao,” anasema.

Aidha, anaeleza wasiwasi wake kuhusu matukio ya baadhi ya walimu kuwapa ujauzito wanafunzi wao.

“Hivi karibuni kulikuwa na tukio mjini Juba ambapo mwalimu alimpa ujauzito mwanafunzi. Mtu aliyepaswa kumlinda mtoto ndiye aliyekuwa akimdhuru,” anasema.

Kwa mujibu wa ripoti za mwaka 2025 za Kundi la Ulinzi dhidi ya Ukatili wa Kijinsia (GBV Protection Cluster), zaidi ya asilimia 52 ya wasichana nchini Sudan Kusini huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Hitimisho: Je, Sera Pekee Zinatosha?

Kutoka Rwanda hadi Tanzania na Sudan Kusini, simulizi za wasichana hawa zinaonesha jambo moja la msingi: ujauzito wa utotoni mara nyingi huwa mwisho wa safari yao ya elimu.

Ingawa serikali za nchi hizi zimeweka sera zinazowaruhusu mama vijana kurejea shuleni, bado umaskini, unyanyapaa, majukumu ya malezi ya watoto, ndoa za utotoni na changamoto za utekelezaji wa sera hizo vinaendelea kuwazuia wengi wao kurejea darasani.

Kwa hiyo, changamoto kubwa inayokabili Afrika Mashariki leo si tu kuzuia mimba za utotoni, bali pia kuhakikisha kuwa ujauzito hauwi sababu ya kumwondolea msichana haki yake ya msingi ya kupata elimu.

Kwa maelfu ya wasichana kama Eugenie, Sandrine, Joyce, Kuruthum, Juan na Kiden, ndoto zao bado zipo.

Makala hii imeandaliwa na Twahirwa Eric kutoka Rwanda, Denis Logonyi kutoka Sudan Kusini na Penina Malundo kutoka Tanzania, kwa msaada wa Fojo Media Institute.