Na Mwandishi wetu, Kigoma
SERIKALI imeendelea kuweka mazingira bora ya kuishi kwa wazee nchini kupitia uboreshaji wa Sera, huduma za afya na ukarabati wa makazi ya wazee ili kuhakikisha wanaishi kwa heshima, usalama na utu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, Julai 14, 2026, alipotembelea Makazi ya Wazee na Wasiojiweza Kibirizi mkoani Kigoma kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa huduma za ustawi wa jamii kwa wazee wanaoishi katika makazi hayo.
“Serikali inatambua wazee kuwa ni tunu, hazina ya hekima na msingi wa maadili ya Taifa letu. Tunathamini mchango wao mkubwa katika ujenzi wa familia, jamii na Taifa, hivyo tutaendelea kuhakikisha wanaishi kwa heshima, usalama na utu, Makazi ya wazee yanapaswa kuwa suluhisho la mwisho pale ambapo mazingira ya kifamilia hayatoi fursa ya kuwahudumia wazee, huku jamii ikiendelea kuthamini na kuwalea wazee ndani ya familia zao ” alisema Naibu Waziri Mahundi.
Aidha, Naibu Waziri Mahundi amesema Wizara imetenga jumla ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa Makazi ya Wazee nchini, ambapo kati ya fedha hizo shilingi milioni 100 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha Makazi ya Wazee Kibirizi ili kuendelea kuwapatia wazee mazingira salama na huduma bora zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, amewapongeza watumishi wanaotoa huduma katika Makazi ya Wazee Kibirizi kwa kujitolea kuwalea na kuwahudumia wazee kwa upendo na heshima na kuhakikisha vituo hivi vinakuwa sehemu salama ambapo wazee wanaishi bila unyonge na wanapata huduma zote stahiki
“Hii ni Wizara inayogusa moja kwa moja maisha na utu wa wananchi niwapongeza watumishi wote wa makazi haya kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwalea na kuwahudumia wazee wetu, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha vituo hivi vinakuwa sehemu salama ambapo wazee wanaishi bila unyonge na wanapata huduma zote stahiki kwakua Hii ni Wizara inayogusa moja kwa moja maisha na utu wa wananchi” amesema Mkuu wa Wilaya Chuachua.
Awali akiwasilisha taarifa ya Makazi ya Wazee na Wasiojiweza Kibirizi, Mfawidhi wa Makazi hayo, Binura Joshua, amesema makazi hayo ni miongoni mwa makazi 13 yanayosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ambapo huduma bora za ustawi wa jamii kwa wahudumiwa wake zinatolewa kikamilifu, zikiwemo huduma za chakula, malazi, afya na ushauri nasaha wa kijamii pia makazi yanashirikiana na Wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa wahudumiwa wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao ya msingi na kuboresha ustawi wao.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee na Wasiojiweza Kibirizi wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuendelea kuwajali na kuwapatia huduma muhimu zinazowawezesha kuishi kwa amani na heshima.
“Tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kutukumbuka na kuendelea kutuhudumia, Pamoja na changamoto za mazingira zilizopo, hatukosi chakula, matibabu na malezi ya upendo kutoka kwa watumishi wa makazi Tunajisikia kuwa sehemu ya familia na tunaendelea kuishi kwa matumaini,” wamesema wazee hao.

More Stories
Halmashauri Nkasi yapongezwa kwa kupata hati safi
Kutofahamika kwa taasisi za uwezeshaji kiuchumi nchini chanzo Cha umasikini
PPRA yashinda Tuzo, yaahidi kuendelea kuhudumia wananchi