Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema itaendelea kutoa elimu na kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na wadau wa sekta ya ununuzi wa umma, baada ya kutwaa tuzo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yaliyohitimishwa Julai 13, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Vicky Morel, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, aliwashukuru Watanzania na wadau wa ununuzi na ugavi kwa ushirikiano wao uliowezesha mamlaka hiyo kupata tuzo katika kundi la waoneshaji waliotoa elimu kuhusu ununuzi wa umma na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa NeST.
Alisema tuzo hiyo ni uthibitisho wa imani ambayo wananchi na wadau wameendelea kuiweka kwa PPRA katika juhudi zake za kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika ununuzi wa umma kupitia matumizi ya teknolojia.
“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA tunawashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kutuunga mkono na kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu. Tunawashukuru pia wadau wa ununuzi na ugavi kwa ushirikiano wao uliotuwezesha kupata tuzo hii katika Maonesho ya Sabasaba,” alisema Mollel.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo yanafuatia hatua nyingine muhimu iliyopatikana hivi karibuni ambapo Mkurugenzi Mkuu wa PPRA aliwakilisha Serikali nchini Uswisi na kupokea tuzo ya kimataifa kwa mfumo wa NeST, uliotambuliwa kuwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali duniani.
Mollel alisema PPRA itaendelea kutumia maonesho na majukwaa mbalimbali kuwafikia wananchi na wadau kwa kutoa elimu kuhusu sheria, kanuni na matumizi ya mfumo wa NeST ili kuongeza uelewa na ushiriki katika ununuzi wa umma.
Alikiri kuwa bado kuna wananchi na wadau wengi ambao hawajafahamu kikamilifu majukumu ya PPRA pamoja na fursa zinazopatikana kupitia mamlaka hiyo, hivyo taasisi itaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi hata baada ya kumalizika kwa Maonesho ya Sabasaba.
“Maonesho haya si mwisho wa utoaji wa elimu. Tutaendelea kuwafikia wananchi na wadau katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanaelewa fursa zilizopo, matumizi ya mfumo wa NeST na umuhimu wa kuzingatia taratibu za ununuzi wa umma,” alisema Mollel.
Alisisitiza kuwa PPRA itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mfumo wa ununuzi wa umma unakuwa wenye uwazi, tija na unaochangia maendeleo ya Taifa.

More Stories
Dkt.Mwinyi awahimiza Wafanyabiashara kutumia fursa za Masoko
Kapinga amwezesha mwenye ulemavu Mashine kusaga viungo
Dkt.Latifa:Sabasaba yafungua milango ya masoko ya Kimataifa