July 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwinyi awahimiza Wafanyabiashara kutumia fursa za Masoko

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wafanyabiashara na wazalishaji nchini kutumia kikamilifu fursa za masoko ya kikanda na kimataifa ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba), Dkt. Mwinyi alisema maendeleo ya sekta ya biashara na viwanda yanategemea matumizi sahihi ya fursa zilizopo pamoja na usimamizi madhubuti wa sera na mipango ya maendeleo.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwa biashara na uwekezaji kupitia utekelezaji wa sera mbalimbali, nidhamu na uwajibikaji, ili kuhakikisha sekta ya biashara na viwanda inaendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Maonesho haya yameonesha wazi kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa wa kujenga uchumi wa kisasa, wenye ushindani na unaotegemea uzalishaji wa ndani,” amesema Dkt. Mwinyi.

Aidha, amewahamasisha wafanyabiashara kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) pamoja na soko la China ambalo limefungua nafasi ya ushuru wa asilimia sifuri kwa baadhi ya bidhaa zinazotoka Afrika.

Ameeleza kuwa matumizi ya fursa hizo yataongeza mauzo ya bidhaa zinazozalishwa nchini, kupanua masoko ya kimataifa na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi.

Dkt. Mwinyi pia amezitaka taasisi za Serikali kuendelea kupunguza urasimu unaochelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi na wafanyabiashara, huku akisisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Vilevile, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuendelea kutafuta masoko mapya na kuimarisha huduma wezeshi zitakazowawezesha Watanzania kunufaika zaidi na fursa za biashara na uwekezaji.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Mwinyi amewapongeza washiriki, waandaaji na wadau wote waliofanikisha Maonesho ya 50 ya SabaSaba, akisema mafanikio hayo yanaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi muhimu kama kitovu cha biashara, uwekezaji na ubunifu barani Afrika.