July 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

MKURUGENZI wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji, amewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, ambayo amesema yanaendelea kuliingizia Taifa gharama kubwa za matibabu.

Dkt. Mbwanji ametoa wito huo Julai 11,2026 wakati wa Tamasha la Michezo la Watumishi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya lililowakutanisha zaidi ya watumishi 1,200. Tamasha hilo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuimarisha mshikamano miongoni mwa watumishi na kuwa mfano kwa jamii katika kuhamasisha mazoezi.

Amesema michezo husaidia kuimarisha afya ya mwili na akili, huku ikiwajengea watumishi ushirikiano na mahusiano mazuri kazini, jambo linalochangia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

“Lengo letu ni kuwaweka watumishi pamoja ili wafahamiane, washirikiane na kudumisha afya zao. Wakiwa na afya njema na ushirikiano mzuri, wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Dkt. Mbwanji.

Ameongeza kuwa sambamba na tamasha hilo, wananchi walipata huduma za uchunguzi wa afya bila malipo, zikiwemo vipimo vya shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa mujibu wa Dkt. Mbwanji, ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza limeendelea kuongeza mzigo wa gharama za matibabu kwa Serikali, taasisi za bima za afya na wananchi kwa ujumla.

Ameeleza kuwa magonjwa hayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na mfumo usiofaa wa maisha, ikiwemo kutofanya mazoezi, ulaji usiozingatia lishe bora pamoja na tabia nyingine zinazohatarisha afya.

“Mazoezi ni sehemu muhimu ya kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza. Tunawasihi wananchi wajenge tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kulinda afya zao na kupunguza gharama za matibabu,” amesema.

Kwa upande wake, mtumishi wa Idara ya Watoto katika hospitali hiyo, Happy Minja, amesema tamasha hilo limekuwa likiwajenga watumishi katika mshikamano, kuwapa nafasi ya kufahamiana zaidi na kuimarisha afya zao kupitia michezo.

Naye Gloria Ayub, ambaye pia ni mtumishi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, amesema michezo imekuwa chachu ya kuimarisha afya za watumishi na kuongeza ushirikiano mahali pa kazi, hali inayochangia utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.