July 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Siku ya Kiswahili duniani yafana nchini Algeria

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Algeria

IMEELEZWA lugha ya Kiswahili inaendelea kukua na kuenea  ambapo sasa inazungumzwa na watu zaidi ya milioni 200 katika nchi 14 duniani na kutumika rasmi katika jumuiya kadhaa za kikanda barani Afrika na kimataifa.

Hayo yamebainishwa  Julai 9,2026 na Balozi wa Tanzania nchini Algeria,Mobhare Matinyi,katika sherehe za siku ya lugha ya Kiswahili duniani, zilizoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria na kufanyika jijini Algiers.Huku  zikihudhuriwa na Mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, taasisi za umma na binafsi, wanazuoni na waandishi wa habari walioongozwa na Katibu Mnadhimu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya Algeria  Nacera Ayaïchia.

Balozi wa Tanzania nchini Algeria Mobhare Matinyi(kulia),akiwa na Katibu Mnadhimu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Sanaa nchini Algeria Nacera Ayaïchia(kushoto)

Balozi Matinyi kupitia hotuba yake ambayo alitumia lugha ya Kiswahili na nakala katika tafsiri ya lugha za Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza kusambazwa kwa wageni waalikwa waliopewa fursa ya kuifuatilia kwa sauti na maandishi kwenye skrini kubwa,amesema mbali  na  Tanzania kutumia lugha hiyo, Kiswahili pia ni lugha ya taifa nchini Kenya, Uganda,Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Amesema  Kiswahili ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika(AU),Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). 

Pia ametaja mifano ya redio za nchi za Uingereza,Ujerumani,Ufaransa,Japan, China, Iran, India na wakati fulani Marekani ambazo hutumia lugha ya Kiswahili katika matangazo yake ya kila siku.

Akirejea kauli mbiu ya mwaka huu ya siku hiyo ya “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi Duniani”, Balozi Matinyi amesema Kiswahili ni lugha ya kujivunia ambayo imetumika katika mapambano ya ukombozi barani Afrika na inaendelea kutumika kulinda amani,kuleta mshikamano na kujenga uchumi barani humo.

Hata  hivyo sherehe hiyo ilinogeshwa na filamu fupi ya dakika kumi iliyoonesha Marais wa zamani na wa sasa wa Tanzania na baadhi wa nchi za Mashariki,Kati na Kusini mwa Afrika wakihutubia kwa lugha ya Kiswahili kwa nyakati tofauti. 

Filamu hiyo pia inamuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan,akihutubia kwa lugha ya Kiswahili nchini Komoro mwaka 2025 kwenye sherehe za miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo.

Balozi wa Tanzania nchini Algeria Mobhare Matinyi( kushoto), akisalimiana na mmoja wa wageni waliohudhuria sherehe za siku ya lugha ya Kiswahili duniani, zilizoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria na kufanyika jijini Algiers.

Huku Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma kwenye vyuo vikuu nchini Algeria, walicheza ngoma mbili za makabila ya Tanzania ya Kimasai na Kihaya na kuimba shairi la Kiswahili.

Aidha sherehe hiyo iliyotumia lugha nne zikiongozwa na Kiswahili,ilipambwa pia na vinywaji vya chai na kahawa ya Tanzania,vyakula vya mapishi ya Kiswahili,maonesho ya mavazi ya wakaazi wa Pwani ya Tanzania kama khanga,baibui,kanzu,vikoi na vitenge yaliyooneshwa na wanafunzi wa Tanzania. 

Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani huadhimishwa Julai tangu mwaka 2022 kufuatia uamuzi wa UNESCO wa mwaka 2021 wa kuitangaza  Julai 7,kuwa siku ya maadhimisho ya lugha hiyo pekee barani Afrika kuwahi kupewa hadhi hii kimataifa.