July 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SMAUJATA waipongeza HGWT kupambana na Ukatili Mara

SMAUJATA Waipongeza HGWT kupambana na ukatili Mara.

Na Fresha Kinasa, TimesmajiraOnline,Mara.

TAASISI ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) imepongeza jitihada zinazofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania la Mkoani Mara katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kusaidia watoto wa kike kutimiza ndoto zao.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii, Hashimu Omary, ameyasema hayo Julai 10, 2026 alipotembelea Kituo cha Nyumba Salama Butiama akiwa na viongozi mbalimbali wa SMAUJATA kutoka ngazi ya Kanda na Mkoa wa Mara.

Kituo cha Nyumba Salama Butiama kinamilikiwa na shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania. Ambapo limeendelea kupambana na ukatili wa kijinsia Mkoani Mara kwa kutoa elimu ya ukatili kwa jamii, makongamano, kutoa msaada kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni.

Akizungumza na wasichana waliopo kituoni hapo, ambao wanapata hifadhi baada ya kukimbia vitendo mbalimbali vya ukatili ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao, Omary amewataka kusoma kwa bidii na kusimamia ndoto zao kwani serikali imeweka mazingira bora kwa kila mtoto kupata elimu.

“Nimpongeze Mkurugenzi wa shirika hili, Rhobi Samwelly, kwa maono yake ya kuanzisha Nyumba Salama hii ambayo imekuwa msaada kwenu. Mnapata hifadhi, mnaendelezwa kielimu, na mnapatiwa mahitaji mbalimbali mkiwa hapa. Someni kwa bidii ili muje kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali na pia muendelee kuwa mabalozi wa kupinga ukatili na kuchochea maendeleo,” amesema Hashimu.

Naye Afisa Mwelimishaji Jamii wa shirika hilo, Emmanuel Good Luck, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly, ameipongeza SMAUJATA kwa kuwatembelea wasichana hao. Amesema, ziara hiyo imewatia moyo wasichana hao na kuwakumbusha kuwa hawako peke yao.

“Tunawashukuru kwa kuwapa ushauri na kuwatia moyo ili wasijione wapweke. Wametambua kuna watu nyuma yao wanaowaombea kwa Mungu baraka na heri ili wahakikishe wanatimiza ndoto zao, kwani,” amesema Good Luck.

Pia, amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi, kwa kuendelea kukemea vikali vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kuhamasisha mabadiliko chanya kwa wananchi ili kuachana na mila potofu na zenye madhara kwa wasichana jambo ambalo limeendelea kuwa na manufaa katika juhudi za kutokomeza ukatili mkoani humo.