Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online
WAKULIMA na wajasiriamali wa zao la korosho wametakiwa kuangalia zao hilo kama malighafi ya kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye thamani badala ya kutegemea uuzaji wa korosho pekee, hatua itakayoongeza kipato, ajira na thamani ya mazao yao.
Wito huo umetolewa na Mkufunzi wa Chuo cha VETA Mtwara kutoka Idara ya Uhandisi wa Mitambo na Umeme, Nestory Agricola, wakati wa mahojiano kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Agricola alisema VETA Mtwara imeshiriki maonesho hayo kwa kuwasilisha ubunifu wa mashine inayoweza kutenganisha tunda la korosho , kokwa zake na bibo huku ikikusanya pia juisi ya tunda hilo kwa ajili ya usindikaji wa bidhaa mbalimbali.
Alieleza kuwa juisi inayopatikana inaweza kusindikwa na kuzalisha mvinyo wa korosho, huku kokwa zikichakatwa katika bidhaa tofauti zenye thamani kubwa sokoni.
“Mbali na korosho za kawaida, tumeleta pia bidhaa mbalimbali zinazotokana na korosho ikiwemo biskuti, siagi ya korosho na keki ya korosho ambayo inaweza kutumika kama kiambato cha vyakula au kupakwa kwenye mkate,” alisema.

Aliongeza kuwa lengo la ubunifu huo ni kuwahamasisha wakulima na wajasiriamali kutambua kuwa zao la korosho lina fursa nyingi za kuongeza thamani kupitia usindikaji badala ya kuuza malighafi pekee.
Kwa mujibu wa Agricola, VETA Mtwara inaendelea kufanya tafiti za kutengeneza mashine nafuu ya kubangua korosho ili kupunguza changamoto zinazowakabili wakulima wakati wa uchakataji wa zao hilo.
“Changamoto ya ubanguaji imekuwa ikiwakwamisha wakulima wengi,ndiyo maana tunaendelea kubuni teknolojia itakayorahisisha kazi hiyo kwa gharama nafuu na kuongeza tija katika sekta ya korosho,” alisema.
Aliwataka wananchi wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Sabasaba kufika katika banda la VETA Mtwara kujionea teknolojia hiyo pamoja na bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la korosho, akisisitiza kuwa ubunifu huo unaweza kuwa chachu ya kuongeza thamani ya mazao, kukuza biashara na kuinua uchumi wa wakulima na wajasiriamali nchini.

More Stories
Kitabu cha Falsafa ya Mama Samia cha zinduliwa
SMAUJATA waipongeza HGWT kupambana na Ukatili Mara
FCC yajipanga kuendelea kulinda ushindani maslahi ya walaji