July 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AGITF yahakikisha mikopo nafuu kwa wakulima

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mfuko wa Udhamini wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) umeahidi kuendelea kushirikiana na taasisi za fedha nchini ili kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata mikopo ya gharama nafuu itakayowawezesha kuongeza uzalishaji, ajira na tija katika sekta ya kilimo.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mtendaji wa AGITF, Mwanahiba Mzee, amesema mfuko huo umeendelea kutekeleza jukumu lake la kuwezesha upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Amesema AGITF hutoa dhamana kwa taasisi za fedha ili ziweze kutoa mikopo kwa wakulima kwa masharti nafuu na riba zinazowawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma hizo.

“Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha wakulima wanapata mikopo ya gharama nafuu ili waweze kuwekeza katika shughuli zao za uzalishaji. Hii inasaidia kuongeza tija, ajira na mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa,” amesema.

Mwanahiba amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mkazo katika kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula pamoja na uchumi wa wananchi.

Ameeleza kuwa wakulima wengi nchini huzalisha mara moja kwa mwaka na hutegemea mavuno yao kwa muda mrefu kabla ya kuanza msimu mwingine wa kilimo, jambo linalowafanya kuhitaji mikopo yenye masharti rafiki na gharama nafuu.

“Ni muhimu mikopo ya kilimo ikazingatia mazingira halisi ya wakulima. Gharama kubwa za mikopo zinaweza kupunguza uwezo wao wa kuendelea kuwekeza na kuongeza uzalishaji,” amesema.

Kwa upande wa mwaka wa fedha 2026/27, ambao ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mwanahiba amesema AGITF imejipanga kuongeza ushirikiano na taasisi za kifedha ili kuhakikisha mikopo inapatikana kwa haraka, kwa wingi na kwa masharti nafuu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima, kuongeza kipato cha kaya, kuchochea ajira na kukuza mchango wa sekta ya kilimo katika maendeleo ya taifa.

Aidha, AGITF imeweka mkazo katika kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji kupitia upatikanaji wa mikopo na mitaji.

“Tumejipanga kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha vijana na wanawake wanapata fursa za kifedha zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi,”amesema.

Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha huduma, bidhaa na fursa mbalimbali zinazolenga kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.