July 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BRELA yawapa elimu ya Urasimishaji Biashara vijana wanaoshiriki Sabasaba

Na Penina Malundo,Timesmajira

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeendelea kuimarisha juhudi za kuwawezesha vijana wajasiriamali kwa kutoa mafunzo ya urasimishaji biashara kwa vikundi vya vijana vinavyoshiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Mafunzo hayo yalitolewa wakati wa ziara ya BRELA katika banda la Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, ambapo vijana walipata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo, ikiwemo usajili wa majina ya biashara, kampuni na ulinzi wa alama za biashara na huduma.

Akitoa mafunzo hayo, Afisa Usajili wa BRELA kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu, Benedickson Willson, amesema elimu hiyo inalenga kuwajengea uwezo wafanyabiashara vijana ili waweze kuendesha biashara zao kwa kufuata misingi ya kisheria na kuongeza ushindani katika soko la ndani na la kimataifa.

Ameeleza kuwa usajili wa biashara na ulinzi wa alama za biashara ni hatua muhimu kwa wabunifu na wajasiriamali wanaotaka kukuza biashara zao kwa usalama na kuzuia matumizi yasiyo halali ya majina au nembo zao.

“Mafunzo haya yanawasaidia vijana kuelewa umuhimu wa kusajili biashara zao na kulinda bunifu zao mapema ili kuepuka changamoto za kisheria na migogoro inayoweza kujitokeza baadaye,” amesema Willson.

Aidha, amesema utoaji wa elimu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Viwanda na Biashara kwa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhakikisha zinawafikia washiriki wa Sabasaba kwa huduma na elimu zinazochochea ukuaji wa biashara.

Baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu namna ya kulinda biashara na bunifu zao kisheria.

“Tumepata maarifa muhimu kuhusu usajili wa biashara na ulinzi wa nembo. Elimu hii itatusaidia kukuza biashara zetu kwa kujiamini na kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye,” amesema mmoja wa washiriki.

BRELA imeendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kama jukwaa la kuwafikia wafanyabiashara na wajasiriamali kwa kutoa huduma za papo kwa papo pamoja na elimu kuhusu huduma zake mbalimbali. Katika mafunzo hayo ya leo, wawakilishi wa vikundi tisa vya vijana kutoka mikoa tofauti nchini walinufaika na elimu hiyo.