Na Joyce Kasiki,Timeamajira online



WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ametembelea banda la Kiwanda cha NIDA katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na utendaji wa kiwanda hicho.
Akiwa katika banda hilo leo Julai 8,2026 Kapinga aliupongeza uongozi wa NIDA kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya viwanda na kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Mahusiano wa NIDA, Mohamed Honelo, alisema kampuni hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kutatua changamoto ya ajira kwa kutoa ajira za moja kwa moja kati ya 1,500 na 2,000, pamoja na ajira za muda kulingana na mahitaji ya uzalishaji.
Alisema kampuni imejenga mnyororo kamili wa uzalishaji unaoanzia kwa kuwawezesha wakulima wa pamba, kununua mazao yao, kuyasindika kuwa nyuzi na vitambaa katika kiwanda chake kilichopo Mbeya, kisha kuvipeleka NIDA Textile Mills kwa ajili ya uchapishaji kabla ya kuviuza kupitia maduka yake.
Kwa mujibu wa Honelo, mfumo huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kuongeza viwanda nchini, kuzalisha ajira, kukuza biashara na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.
Aliongeza kuwa bidhaa za kampuni hiyo, zikiwemo kanga, vitenge, mashuka na bidhaa nyingine zinazotokana na pamba, zinapatikana katika maduka ya NIDA na NIDA Textile Mills, huku akiwakaribisha wananchi kuzinunua na kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini.
Aidha, Honelo aliiomba Serikali kuweka utaratibu utakaowezesha sehemu kubwa ya pamba inayozalishwa nchini kubaki kwa matumizi ya viwanda vya ndani badala ya kuuzwa nje kama malighafi.
“Tunaiomba Serikali iweke akiba ya pamba kwa ajili ya viwanda vya ndani. Ni kweli hatuwezi kununua pamba yote kwa wakati mmoja, lakini kiasi kinachobaki kihifadhiwe ili baadaye viwanda vya ndani viweze kukinunua badala ya kulazimika kuagiza au kununua pamba hiyo hiyo kwa gharama kubwa kutoka nje,” alisema Honelo.
Alisema pia gharama kubwa za uzalishaji zinapunguza uwezo wa viwanda vya ndani kushindana na bidhaa kutoka nje, huku wazalishaji wa nchi nyingine wakinufaika na gharama ndogo za uzalishaji zinazowaruhusu kuuza bidhaa kwa bei nafuu zaidi.
Kwa upande mwingine, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuhamasisha maendeleo ya sekta ya viwanda, akisema hatua hiyo itaongeza ajira, kukuza uchumi na kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye msingi imara wa viwanda.

More Stories
Waziri Mkuu mgeni rasmi uzinduzi wa kitabu cha “Mama Samia Doctrine of Law”
Serikali yaahidi kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI
TARI Selian yawaalika wakulima maonesho ya Kilimo-biashara