July 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBA yakaribisha wawekezaji ujenzi makazi bora

Na Joyce Kasiki, Dar es Salaam

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya serikali na makazi ya gharama nafuu huku ukiwahimiza wawekezaji kushirikiana na serikali katika kuongeza upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Hayo yamesemwa na Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa TBA Julai 7,2026 , Renatus Sona, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Sona amesema TBA imejikita katika maeneo mawili makuu ya kuwahudumia wananchi ambapo alisema eneo la kwanza ni ujenzi wa majengo ya serikali yanayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, huku eneo la pili likiwa ni ujenzi wa nyumba za makazi ya gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata makazi bora.

Amesema wakala huo umeanza utekelezaji wa mradi wa nyumba za gharama nafuu katika eneo la Temeke, Dar es Salaam, ukiwalenga wananchi wasioweza kumudu gharama za kununua viwanja au kujenga nyumba kwa uwezo wao.

“Malengo yetu ni kuwa daraja la kuwawezesha wananchi kupata makazi bora kwa gharama nafuu na hivyo kuboresha maisha yao pamoja na kuchochea maendeleo ya Taifa kupitia sekta ya makazi,” alisema Sona.

Aidha, amewataka wawekezaji kushirikiana na TBA katika kuendeleza miradi ya nyumba na majengo ili kuongeza upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi na kuunga mkono jitihada za serikali katika maendeleo ya sekta ya ujenzi.

Naye Msanifu Majengo wa TBA, Stanley Hashim, amesema ubunifu katika usanifu wa majengo una nafasi kubwa katika kuhakikisha nyumba zinazojengwa zinakuwa salama, zenye ubora na zinazokidhi mahitaji ya kisasa.

Ameeleza kuwa usanifu huzingatia vipengele mbalimbali ikiwemo mpangilio wa madirisha, milango, matumizi sahihi ya nafasi na ubunifu wa kitaalamu unaofanya majengo kuwa ya kisasa, yenye kuvutia na kudumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Henry Staina, Mhandisi wa TBA , amesema wakala huo unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya makazi katika mji wa serikali wa Mtumba, ikiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba 350 katika eneo la Nzuguni.

Amesema awamu ya kwanza ya mradi huo ilihusisha ujenzi wa nyumba 150 ambazo tayari zimekamilika na watumishi wa umma wamekwishaanza kuishi katika nyumba hizo.

Staina amesema awamu ya pili, iliyoanza mwaka 2020, inaendelea ambapo nyumba nyingine 150 pamoja na jengo la ghorofa lenye vyumba 30 vinaendelea kujengwa na baadhi ya kazi zimefikia hatua za mwisho za ukamilishaji.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma na wakazi wa Mkoa wa Dodoma kwa ujumla, kwa kuwa nyumba hizo zinapatikana kwa gharama nafuu zinazoweza kumuduwa na watumishi.

“TBA itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na sekta binafsi kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na salama, sambamba na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za umma kupitia ujenzi wa majengo ya kisasa,” amesema Staina.

” Ushirikiano kati ya serikali na wawekezaji ni nguzo muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi, kukuza sekta ya ujenzi na kuharakisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Taifa.”amesisitiza