Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Mbeya
MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya shilingi trilioni 3.9 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa miundombinu ya Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), hatua inayolenga kuboresha huduma za usafiri wa reli na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Itunda ametoa kauli hiyo Julai 6, 2026,wakati alipokuwa akifungua maadhimisho ya Wiki ya Miaka 50 ya TAZARA yaliyofanyika jijini Mbeya.
Amesema uwekezaji huo mkubwa unaonesha dhamira ya Serikali ya kuifanya TAZARA kuwa reli yenye ufanisi mkubwa katika usafirishaji wa mizigo na abiria ndani na nje ya Tanzania.
“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazoendelea kuzifanya katika kuimarisha miundombinu ya reli uwekezaji huu utaiwezesha TAZARA kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na wafanyabiashara,” amesema Itunda.

Ameongeza kuwa fedha hizo zitasaidia kuboresha miundombinu ya reli, kuongeza usalama wa safari na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na abiria, jambo litakalochangia kukuza biashara na maendeleo ya uchumi wa Taifa.
“Sio jambo dogo Serikali kutenga kiasi hiki cha fedha kwa ajili ya ukarabati wa TAZARA. Huu ni uwekezaji wenye manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa TAZARA uliopo Kata ya Iyunga na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya usafirishaji pamoja na wananchi waliojitokeza kusherehekea miaka 50 ya shirika hilo.
Katika hotuba yake, Itunda pia amepongeza menejimenti ya TAZARA, ikiongozwa na Kaimu Meneja wa Mkoa, kwa juhudi wanazozifanya kuhakikisha shirika linaendelea kutoa huduma bora na kuongeza ufanisi wa shughuli zake.
Aidha, amewataka wananchi kushiriki kulinda miundombinu ya reli kwa kuepuka vitendo vya uharibifu na wizi wa vifaa vya reli, akisisitiza kuwa reli hiyo ni mali ya umma inayochangia maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo walieleza kuwa TAZARA imekuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Mbeya.

Mkazi wa Ituta, Hassan Juma, alisema uwepo wa reli hiyo umefungua fursa nyingi za biashara na ajira kwa wananchi.
Naye Lucy Kisanji, mkazi wa Iyunga, alisema wananchi wataendelea kushirikiana na Serikali kulinda miundombinu ya TAZARA na kutoa elimu dhidi ya vitendo vya wizi wa vyuma vya reli vinavyouzwa kama vyuma chakavu.
Maadhimisho ya miaka 50 ya TAZARA yanalenga kutathmini mafanikio ya shirika hilo tangu kuanzishwa kwake pamoja na kujadili mikakati ya kuimarisha huduma za usafiri wa reli katika siku zijazo.

More Stories
TBA yakaribisha wawekezaji ujenzi makazi bora
Bodi ya Mkonge yahamasisha uwekezaji zao la Mkonge
Tamasha la Kimataifa Sanaa na Utalii kufanyika Oktoba