July 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbegu Bora nguzo ya kuongeza tija ya Kilimo

Na Joyce Kasiki ,Timesmajira online

WAKULIMA nchini wamehimizwa kutumia mbegu zenye ubora uliothibitishwa ili kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza kipato chao, huku Taasisi ya Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI) ikiendelea kusimamia viwango vya ubora wa mbegu zinazotumika nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkaguzi wa Mbegu kutoka TOSCI, Fatma Nassoro, alisema taasisi hiyo inahakikisha mbegu zote zinazowafikia wakulima zinakidhi viwango vinavyotakiwa kupitia ukaguzi na uthibitishaji wa kitaalamu.

Alieleza kuwa TOSCI hufanya ukaguzi wa mashamba ya wazalishaji wa mbegu, hujaribu aina mpya za mbegu na kufanya uchunguzi wa maabara ili kuthibitisha ubora wake kabla ya kuruhusiwa kuingia sokoni.

Aidha, alisema taasisi hiyo huendesha mafunzo kwa wazalishaji wa mbegu na wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo ili kuwajengea uwezo wa kuzingatia viwango vinavyohitajika katika uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora.

Fatma aliongeza kuwa ukaguzi pia hufanyika katika maduka ya pembejeo na maghala ya kuhifadhi mbegu, ambapo sampuli huchukuliwa kwa ajili ya vipimo vya maabara ili kuhakikisha ubora wake unaendelea kukidhi viwango.

Alifafanua kuwa maabara ya TOSCI, iliyoanzishwa mwaka 2003 na kuboreshwa mwaka 2023, imeongeza uwezo wa taasisi katika upimaji na uthibitishaji wa mbegu kwa ufanisi zaidi.

Pia aliwahimiza wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kutembelea banda la TOSCI ndani ya eneo la Wizara ya Kilimo kwenye maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu uzalishaji wa mbegu bora, matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na taratibu za usajili wa wazalishaji wa mbegu.

Alisisitiza kuwa matumizi ya mbegu bora ni hatua muhimu katika kuongeza tija ya kilimo na kuchangia maendeleo ya uchumi wa mkulima na Taifa kwa ujumla.