July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpogolo: Hali ya usalama Ilala ni shwari

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema hali ya usalama katika wilaya hiyo ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani na utulivu kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka unaoenda sambamba na uchaguzi Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Mpogolo amesema uongozi wa Wilaya ya Ilala chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam unaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama na kuhakikisha amani inadumishwa wakati wote.

Amewashukuru Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao.

“Sisi kama Wilaya ya Ilala tunawafahamisha wananchi kwamba hali ya usalama ni nzuri. Tunavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuimarisha usalama na kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa utulivu,” amesema.

Mpogolo amesema wananchi wanapaswa kuendelea kusherehekea na kutafakari Siku ya Sabasaba kwa amani huku wafanyabiashara wakiendelea kufanya shughuli zao bila hofu.

Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.

“Tunawaomba wananchi wawe sehemu ya ulinzi wa nchi yetu. Mtu yeyote anapoona viashiria vya uvunjifu wa amani atoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua zichukuliwe kwa wakati,” amesema.

Pia amesema viongozi wa Serikali za Mitaa wamehimizwa kuendelea kuwa macho na kushirikiana na wananchi katika kulinda usalama wa maeneo yao, akisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi.

Amesema ushirikiano kati ya wananchi, viongozi wa Serikali za Mitaa na vyombo vya ulinzi na usalama ni nguzo muhimu katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu nchini.