July 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaouza sarafu waonywa

Na Joyce Kasiki, Dar es Salaam

BENKI Kuu ya Tanzania  imeeleza kuwa biashara ya kuuza na kununua  sarafu za Tanzania ni haramu kwa kuwa haitambuliki kisheria na mtu yeyote atakayebainika kujihusisha nayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hayo yameelezwa Julai 4,2026 na Afisa kutoka Kurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu Benki Kuu ya Tanzania (BoT),  Shadrack Mapunda wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alifafanua majukumu ya Benki Kuu katika uzalishaji na usambazaji wa noti na sarafu nchini.

Alisema Benki Kuu ndiyo yenye jukumu la kutengeneza na kusambaza noti na sarafu zote zinazotumika nchini, huku usambazaji kwa wananchi ukifanyika kupitia benki za biashara.

“Benki Kuu inasambaza noti na sarafu kwa benki za biashara. Mwananchi anayehitaji noti au sarafu anatakiwa kuzipata kupitia benki yake ya biashara kwa kuwa ndizo zinazopokea fedha hizo kutoka Benki Kuu na kuzisambaza kwa wateja,” alisema Mapunda.

Baadhi ya wananchi wakiwa katika banda la BoT kwenye foleni ya kuchukua chenchi

Akizungumzia malalamiko ya wananchi kuhusu upatikanaji wa chenji, Mapunda alisema BoT huendelea kuzisambaza kwa benki za biashara kwa kiwango kinachohitajika, hivyo wananchi wanapaswa kuzipata kupitia taasisi hizo za kifedha.

Alieleza kuwa Benki Kuu ni Benki ya benki za biashara, hivyo benki hizo hupata huduma za kutoa na kuweka fedha pamoja na noti na sarafu kutoka BoT kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Kuhusu watu wanaouza noti au sarafu kwa bei ya juu kuliko thamani yake, Mapunda alisema shughuli hiyo si biashara halali kwa kuwa haijatambuliwa katika sheria za usajili wa biashara nchini.

“Ukiangalia orodha ya biashara zinazotambulika kisheria nchini, huwezi kukuta biashara ya kuuza na kununua noti au sarafu za Tanzania. Hivyo anayejihusisha na biashara hiyo anafanya biashara haramu kwa kuwa hana kibali chochote cha kisheria,” alisema.

Aliongeza kuwa tofauti na biashara ya ubadilishaji fedha za kigeni inayofanywa na taasisi zilizopewa leseni, biashara ya kuuza noti na sarafu za Tanzania haina utaratibu wala kibali cha kisheria.

Mapunda alitoa rai kwa wananchi kuacha kujihusisha na biashara hiyo akisisitiza kuwa yeyote atakayebainika atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

“Sheria ziko wazi,mtu yeyote anayeendesha biashara ambayo haina kibali anakiuka sheria za nchi na akibainika atachukuliwa hatua za kisheria na Mahakama inaweza kutoa adhabu kulingana na masharti yaliyowekwa kwenye sheria,” alisema.

Alisisitiza kuwa BoT itaendelea kuhakikisha noti na sarafu zinapatikana kwa wakati kupitia benki za biashara ili kurahisisha shughuli za malipo ya bidhaa na huduma kwa wananchi nchini.