Na Joyce Kasiki
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu kishiriki Cha Dar Es Salaam (UDSM) Mkwawa University College of Education (MUCE) amefanya vizuri katika mashindano ya tafiti za wanafunzi wa vyuo vikuu baada ya kushika nafasi ya pili kwa utafiti unaotumia kompyuta maabara kubaini dawa zinazoweza kutumika kutibu magonjwa ya afya ya akili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika bada la UDSM wanafunzi huyo alisema mradi wake ulitumia teknolojia ya kompyuta maabara kuiga mazingira ya mwili wa binadamu ili kuchunguza namna ugonjwa unavyoathiri mwili na kutathmini uwezo wa dawa mbalimbali kushirikiana na protini zinazohusika na ugonjwa huo.
Alisema baada ya kuchunguza misombo mingi ya dawa kwa kuzingatia kanuni za kisayansi, utafiti wake ulibaini dawa tano zenye uwezo wa kuendelea na hatua za majaribio ya kitabibu (clinical trials).
“Nilitumia kompyuta maabara kuiga mazingira ya mwili wa binadamu na kufanya uchambuzi wa dawa mbalimbali. Mwishoni mwa utafiti tulipata dawa tano zinazoweza kuendelea na hatua za majaribio ya kitabibu,” alisema.
Alieleza kuwa lengo la utafiti huo lilikuwa ni kutafuta dawa salama zaidi za kutibu magonjwa ya afya ya akili kutokana na changamoto zilizopo katika baadhi ya dawa zinazotumika sasa, ikiwemo kiwango kikubwa cha sumu kinachoweza kusababisha madhara kama magonjwa ya moyo, saratani na mzio.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, utafiti huo pia ulitathmini namna dawa hizo zinavyoingiliana na protini za mwili zinazohusishwa na ugonjwa ili kubaini kama zinaweza kubaki na ufanisi bila kusababisha mabadiliko yanayoweza kuathiri tiba.
Aidha, alisema utafiti huo ulisimamiwa na Dkt. Pollu Chemba, Mtafiti anayejihusisha na tafiti za kompyuta maabara katika sayansi ya tiba. Aliongeza kuwa matokeo ya utafiti huo tayari yanapatikana mtandaoni katika mfumo wa preprint na yanatarajiwa kuchapishwa rasmi katika jarida la kisayansi.
Mafanikio hayo yalimwezesha kushika nafasi ya pili katika mashindano ya tafiti za wanafunzi wa vyuo vikuu, huku utafiti wake ukitajwa kuwa miongoni mwa miradi bora iliyowasilishwa mwaka huu.

More Stories
Mbibo:Boresheni utoaji leseni za Madini kupunguza Migogoro
Tanzania yapiga hatua kuelekea Uzalishaji wa Umeme wa Nyuklia
Wanaouza sarafu waonywa