Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imezindua rasmi shughuli za Kijiji cha Bima katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam maaraufu kama maonyesho ya Sabasaba.
Uzinduzi huo umeongozwa na Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, na umehudhuriwa na viongozi wa kampuni za bima, madalali wa bima, watoa huduma na wadau mbalimbali wa sekta ya bima hapa nchini.
Kijiji cha Bima ni jukwaa la kila mwaka linaloratibiwa na TIRA kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya bima kwa lengo la kuwasogezea wananchi elimu ya bima, ushauri wa kitaalamu na huduma mbalimbali za bima katika eneo moja.

Kupitia jukwaa hilo, wananchi hupata fursa ya kujifunza umuhimu wa kuweka bima aina mbalimbali kwa lengo la kulinda maisha, afya, mali, biashara na uwekezaji wao kwa ujumla.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Saqware, amesema kukua kwa sekta ya bima kunategemea sana uelewa wa wananchi kuhusiana na dhana nzima ya bima.
Amesema jambo hilo linahitaji ushirikiano mkubwa wa wadau wote katika kuhakikisha elimu na huduma za bima zinawafikia Watanzania wengi zaidi.

Aidha Ametoa wito kwa wananchi kutembelea Kijiji hicho cha Bima kilichozinduliwa ili kupata elimu sahihi inayohusiana na maswala yote ya bima pamoja na kuwa nafasi ya kuchagua aina ya bima ambazo watazihitaji.
Kwa upande wake, uongozi wa TIRA umeeleza kuwa ushiriki wake katika Maonesho ya Sabasaba unaendana na dhamira ya kuongeza uelewa wa umma kuhusu bima katika kukuza ujumuishi wa huduma za kifedha na kuimarisha mchango wa sekta ya bima katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi huo katika kipindi chote cha maonesho, wananchi watapata huduma za ushauri, elimu ya bima, ufafanuzi wa bidhaa mbalimbali za bima pamoja na nafasi ya kukutana ana kwa ana na makampuni yanayojishughulisha na huduma za bima pamoja na wadau wengine walioko kwenye sekta hiyo.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa uongozi wa TIRA unaendelea kuhimiza wananchi kutumia huduma za bima kama nyenzo muhimu ya kudhibiti vihatarishi na kujenga ustahimilivu wa kifedha kwa watu binafsi, biashara na taasisi.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kusimamia, kuendeleza na kuhakikisha sekta ya bima inakuwa imara, shindani katika shughuli zinazohusiana na maswala ya bima kwa ujumla pamoja na inayolinda maslahi ya watumiaji wa huduma za bima.

More Stories
Mixx,Serikali ya Z’bar kushirikiana kuleta mapinduziya kidijitali
TCPM yatoa elimu kuhusu faida za nguzo za zege
Walipakodi wahimizwa kutumia usuluhishi kutatua migogoro ya kodi