July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCPM yatoa elimu kuhusu faida za nguzo za zege

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

Kampuni ya Kutengeneza Nguzo za Zege Tanzania (TCPM) imeendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nguzo za zege katika maendeleo ya sekta ya nishati na miundombinu nchini.

Elimu hiyo inatolewa katika banda la kampuni hiyo lililopo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, ambapo wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu mradi wa uzalishaji wa nguzo za zege na mchango wake katika kuimarisha huduma za miundombinu.

Akiongoza timu ya TCPM katika maonesho hayo, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Mha. Khadija Abdallahmed, amesema kampuni imejikita katika kutoa uelewa kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu faida za matumizi ya nguzo za zege ikilinganishwa na nguzo za miti.

Amesema nguzo za zege zina uimara mkubwa, hudumu kwa muda mrefu, zina uwezo wa kuhimili mazingira mbalimbali na huchangia kupunguza utegemezi wa rasilimali za misitu, hivyo kuwa suluhisho endelevu kwa miradi ya nishati na miundombinu.

Kwa mujibu wa TCPM, ushiriki wake katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono azma ya Serikali ya kuimarisha sekta ya viwanda kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na bidhaa zinazozalishwa nchini.

Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu bidhaa na huduma zake ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia sekta ya viwanda.

Maonesho ya Sabasaba mwaka huu yamefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na yanaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, huku yakiendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda nchini.