Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Mhandisi Richard Mwanja, amewakaribisha wananchi pamoja na wadau wa maendeleo kutembelea banda la kampuni hiyo lililopo ndani ya banda la TANESCO ili kujionea na kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya umeme nchini.
Akizungumza leo, Julai 3, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, Mhandisi Mwanja, amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kufahamu hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya umeme inayolenga kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya jamii.
Mhandisi Mwanja amesema ETDCO inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu ya umeme nchini kwa mafanikio makubwa, huku akieleza kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa njia ya umeme ya kusafirisha umeme kutoka Urambo Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilomita 280.

Kwa upande wao, wananchi waliotembelea banda la ETDCO wamepongeza utekelezaji wa miradi hiyo, wakieleza kuwa umeongeza upatikanaji wa huduma za umeme na kuchangia maendeleo ya taifa.
Maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo, “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania,” sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo.


More Stories
Wizara yahamasisha Watoto kuhusu Nishati Safi
Balozi Omar akoshwa na usimamizi Matumizi ya Moduli
Masaju apongeza kazi ya OSHA