July 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mipango haiwezekani bila Takwimu



Na Joyce Kasiki


DAR ES SALAAM: Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Munde, amesema takwimu sahihi ni msingi muhimu wa kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta mbalimbali hayawezi kupatikana bila kuwa na takwimu za kuaminika.


Akizungumza leo Julai 3,2026 alipotembelea banda la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika maonyesho ya Kimataifa ya Biashara , Naibu Waziri huyo alisema Serikali inaendelea kuthamini mchango wa taasisi hiyo katika kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu zinazosaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa maendeleo ya wananchi.


“Mipango yetu haiwezi kwenda bila takwimu. Takwimu ndizo msingi wa kupanga, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” alisema Munde.


Aidha, aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuhakikisha taifa linapata takwimu sahihi, za wakati na zenye ubora, huku akiwataka watumishi wa taasisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.


Ziara ya Naibu Waziri huyo katika banda la Ofisi ya Taifa ya Takwimu ililenga kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo pamoja na kupata ufafanuzi kuhusu mchango wa takwimu katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.