Na Joyce Kasiki
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Musa Omar ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa hatua inazoendelea kuchukua za kuweka machapisho yake kwenye mfumo wa kidijitali ili yaweze kupatikana kwa urahisi mtandaoni, akisema hatua hiyo itaiwezesha dunia kupata taarifa sahihi za takwimu za Tanzania.
Waziri huyo alitoa pongezi hizo leo Julai 2,2026 jiji Dar Es Salaam alipotembelea banda la NBS katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, jijini humo.
Alisema upatikanaji wa taarifa za NBS mtandaoni ni jambo muhimu katika zama za teknolojia ya akili bandia (AI), kwani watumiaji wengi duniani hutafuta taarifa kupitia mifumo hiyo badala ya kutembelea taasisi husika moja kwa moja.
“Taarifa za NBS kuwepo online zitakuwa zimeisaidia dunia,hongereni, hiyo ni kazi kubwa na muhimu sana maana siku hizi tukitaka taarifa hatuanzi kuzitafuta NBS kwanza, tunaenda kwenye AI,ukiuliza chochote ilimradi kiwepo kwenye mtandao, utapata majibu,” alisema Waziri huyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya NBS alizungumzia kuhusu uwepo wa sera kwenye mambo yanayohusu upatikanaji na matumizi ya taarifa jambo ambalo liliungwa mkono na Balozi Omar ambapo amesema yatafanyiwa kazi kwa ushirikiano kati ya NBS na Wizara ya Fedha mara baada ya maandalizi kukamilika.
“Kwa sasa bado tupo kwenye maandalizi ya sera kuhusu uoatikanaji wa taarifa hizi na tutakapokuwa tayari jambo hili tutalileta kwenu
Naye Mkutubi Ofisi ya Taifa ya Takwimu Issa Magabiro alisema taasisi hiyo inaendelea na zoezi la kuweka kwenye mfumo wa kidijitali machapisho yote ya takwimu, ikiwemo ya miaka ya nyuma kuanzia mwaka 1938 hadi sasa.
Alieleza kuwa kwa sasa machapisho mengi ya zamani bado yapo katika nakala ngumu hivyo yanaendelea kufanyiwa uchanganuzi wa kidijitali ili yaingizwe kwenye mfumo, huku machapisho yote yaliyokuwa katika mfumo wa kielektroniki tayari yakiwa yamehifadhiwa mtandaoni.
Magabiro alisema hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa takwimu rasmi za Taifa kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi, sambamba na kuimarisha uhifadhi wa kumbukumbu muhimu za takwimu za Tanzania.

More Stories
TOSCI Yahimiza Matumizi ya Mbegu Zilizohakikiwa
Wanawake wanufaika zaidi ya Asilimia 51 mikopo SELF
Waziri Kapinga apongeza mafanikio ya TTCL