July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mlipuko wa baruti wasababisha kifo,majeruhi saba 

Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online- Mwanza

MLIPUKO wa baruti uliotokea leo Julai 1,2026 umeacha manjozi kwa wakazi wa mtaa wa Sahwa ya Juu wilayani Nyamagana mkoani Mwanza baada ya kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi saba.

Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa Julai 1,2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbrod  Mutafungwa, mlipuko huo ulitokea majira ya saa 12:46 asubuhi kwenye kibanda cha kahawa Mtaa wa Sahwa ya Juu, Kata ya Lwanhima wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.

DCP.Mutafungwa amesema ​aliyefariki  katika ajali hiyo ni Marco Msenyere (52), mpasua mawe na mkazi wa Semba-Lwanhima,ambapo  wakati wa tukio hilo, marehemu alikuwa na wenzake wakinywa kahawa kwenye kibanda hicho akiwa na begi dogo ambalo ndani yake lilikuwa na baruti hizo.

Ametaja chanzo cha mlipuko huo ni uzembe wa utunzaji wa baruti,kwani  marehemu alibeba baruti hizo na kukaa nazo karibu na jiko la mkaa lililokuwa linawaka kwenye kibanda hicho cha kahawa huku akifahamu wazi kuwa baruti hizo zikipata joto hulipuka.

Pia ametaja majeruhi katika tukio hilo ni  Daudi Baraka muuza kahawa,​Emmanuel Joseph  na ​Yusufu Nasoro  wawili hawa ni fundi ujenzi pamoja na Zawadi Ndukeji mama lishe.

Huku wengine  ni James  Ntugo  na Joseph Englibert  wote hawa ni fundi ujenzi pamoja na Marco Mahunge Chandanoba  ambaye ni mpasua mawe.

Hata hivyo DCP. Mutafungwa amesema eneo la tukio limeshakaguliwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wataalamu wengine, wakiwemo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Maofisa kutoka Tume ya Madini Mwanza na wamejiridhisha kuwa lipo salama kwa matumizi ya wananchi. 

Aidha ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi kutoa taarifa kwa jeshi hilo kuhusu watu wanaotumia na kumiliki baruti pasipo kuwa na kibali,huku akiwataka Wenyeviti wa Mitaa kufanya ukaguzi ili kuwabaini watu hao katika mitaa yao.

​Kwa upande wake Ofisa kutoka Tume ya Madini Mkoa wa  Mwanza, Deus Makuli, amesema ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kumiliki baruti bila kuwa na leseni huku akidai kuwa marehemu alikuwa akimiliki baruti hizo bila kuwa na vibali.

​Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kuhakikisha watu hawafanyi shughuli za kuripua mawe bila kuwa na vibali,hivyo wakiwabaini watoe taarifa kwa vyombo husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

​Nao baadhi ya wananchi wa Lwanhima, akiwemo Mahuma Mungu,wameeleza kusikitishwa na tukio hilo na wameahidi kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wanaotumia vilipuzi kwa ajili ya kulipua mawe katika maeneo yao bila kuwa na vibali halali ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

​Hata hivyo majeruhi katika ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana Butimba na mmoja amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi.