Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetajwa kuwa miongoni mwa taasisi muhimu zinazochangia upatikanaji wa ujuzi na ajira kwa vijana nchini kupitia mafunzo ya vitendo yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda.
Kutokana na mchango huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, aliihimiza VETA pamoja na taasisi nyingine za mafunzo ya ufundi kutumia Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuonesha ubunifu, teknolojia na ujuzi unaozalisha ajira na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania.
Akizungumza baada ya kukagua maandalizi ya maonesho hayo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Balozi Salum alisema maandalizi yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 99 na kwamba Serikali inatarajia maonesho ya mwaka huu kuwa miongoni mwa yenye mafanikio makubwa.

Amesema taasisi za mafunzo kama VETA zina nafasi muhimu ya kuandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.
Amebainisha kuwa maonesho hayo yanapaswa kutumiwa si kwa ajili ya kuuza bidhaa pekee, bali pia kujenga ushirikiano wa kibiashara, kutafuta masoko mapya na kuonesha uwezo wa Watanzania katika ubunifu na uzalishaji wa bidhaa zenye viwango vya kimataifa.

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameeleza kuridhishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini, hususan zile zinazotengenezwa na wajasiriamali wanawake, akisema zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa katika ubora na vifungashio na sasa zinaweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wazalishaji, wajasiriamali na taasisi za mafunzo ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania, kukuza ajira na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

More Stories
TTCL yajipanga kuwahudumia wateja Sabasaba 2026
TTCL yatwaa Tuzo na kutoa gawio Serikalini
Mahundi ahimiza wanawake kutumia kuinua uchumi