June 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendeleza ujenzi  Miundombinu ya Elimu Nanyumbu

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imesema itaendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, ambapo katika mwaka wa fedha 2026/27 imetenga shilingi milioni 380 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na kukamilisha maabara.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri ,Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI) Dkt Jaffar Seif alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu,  Yahya Mhata, ambaye alitaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa shule nne mpya za sekondari katika halmashauri hiyo.

“Je lini Serikali itaanza ujenzi wa shule nne mpya za sekondari katika Halmashauri ya Nanyumbu”amehoji Mhata


Waziri anesema Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu ina jumla ya kata 17 na shule za sekondari 22, huku akibainisha kuwa hakuna kata hata moja isiyo na shule ya sekondari.

Seif ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2025/26, Serikali ilitoa shilingi bilioni 5.56 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika halmashauri hiyo.

Amesema Fedha hizo zilitumika kujenga shule mpya sita za sekondari, madarasa 107, mabweni 13, maabara 10, matundu ya vyoo 78 pamoja na kukarabati madarasa tisa na hosteli mbili.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali imetenga shilingi milioni 560.55 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika Kata ya Kilimahewa.

Ameongeza kuwa fedha zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 zitatumika kujenga madarasa tisa, nyumba mbili za walimu, matundu mawili ya vyoo na kukamilisha maabara mbili, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Wilaya ya Nanyumbu.