June 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPRA yongeza fursa za Makundi Maalum nchini

Na Joyce Kasiki,Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Denis Simba , amesema kuwa serikali imeendelea kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za ununuzi wa umma kupitia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 pamoja na kanuni zake, kwa lengo la kuongeza ushiriki wa makundi maalum katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Akizungumza  katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika uwanja wa Chinangali Park jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema PPRA imekuwa ikitumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika mfumo wa ununuzi wa umma, hususan kwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Simba amesema  kuwa mafanikio hayo yametokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alielekeza kufanyika kwa maboresho ya sheria ya ununuzi wa umma ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki katika fursa za kiuchumi zinazotokana na matumizi ya fedha za umma.

“Sheria hii mpya imeweka utaratibu unaozitaka taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalum ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. Hii ni fursa kubwa sana kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo ya Taifa,” amesema Simba

Simba amebainisha kuwa kwa kuzingatia ukubwa wa bajeti ya serikali na kiwango kikubwa cha fedha kinachotumika katika ununuzi wa umma, fursa zinazopatikana kwa makundi hayo ni kubwa na zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato cha wananchi pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema hadi sasa zaidi ya vikundi 8,700 vimeshajisajili katika mfumo wa kitaifa wa ununuzi wa umma kwa njia ya kielektroniki (NeST), huku lengo likiwa kufikia vikundi 10,000 kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha.

Aidha, amesema thamani ya zabuni zilizotolewa kwa makundi maalum imefikia takribani shilingi bilioni 50, huku mikataba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 45 ikiwa tayari imetolewa na mingine kuanza kutekelezwa.

“Miaka miwili iliyopita tulikuwa tunazungumzia zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni tano hadi sita, lakini leo tumefikia zaidi ya bilioni 50. Haya ni mafanikio makubwa yanayoonyesha dhamira ya serikali ya kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa taifa,” alisema Simba

Simba amewahimiza wananchi kujiunga katika vikundi rasmi na kujisajili kupitia mamlaka za serikali za mitaa ili waweze kutambuliwa na kusajiliwa katika mfumo wa NeST, hatua itakayowawezesha kushiriki katika zabuni zinazotangazwa na zaidi ya taasisi 1,300 za umma nchini.

Pia ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuwa daraja kati ya taasisi za umma na wananchi kwa kusambaza taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo, ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata uelewa na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa sera na mipango ya serikali.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu huyo aliwataka wadau wa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kushiriki katika Kongamano la Ununuzi wa Umma la mwaka 2025 litakalofanyika jijini Arusha mwishoni mwa mwezi Julai, ambapo wadau mbalimbali watapata fursa ya kujadili maendeleo, changamoto na maboresho ya mfumo wa ununuzi wa umma nchini.

Amesisitiza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi mwenye uwezo, maarifa na dhamira ya kufanya biashara na serikali anapata nafasi ya kushiriki katika fursa hizo kwa usawa, hivyo kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.