June 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mil.80 kujenga stendi  ya malori 

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imetenga kiasi  cha sh.milioni 80  mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya maegesho ya malori katika Bonde la Songwe, ikiwa ni  jitihada za kuondoa maegesho holela yanayohatarisha usalama wa watumiaji wa barabara katika Mji wa Mbalizi.

Hatua hiyo inakuja kufuatia ongezeko la malori yanayoegeshwa kiholela kando ya barabara kuu, hali inayosababisha ufinyu,msongamano wa magari na kuhatarisha usalama wa wananchi pamoja na watumiaji wengine wa miundombinu hiyo.

Akizungumza Juni 24, 2026 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha  halmshauri hiyo,kilichojadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2025, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Aida Haule, amesema mradi huo utasaidia kuondoa adha inayowakabili wananchi kutokana na malori kuegeshwa hovyo katika maeneo yasiyo rasmi.

Haule amesema maegesho hayo yamekuwa yakisababisha usumbufu  kwa watumiaji wa barabara, wakiwemo madereva wa vyombo vingine vya moto na watembea kwa miguu, huku wakati mwingine yakichangia kutokea kwa ajali za barabarani.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unatokana na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Beno Malisa, ambaye aliitaka halmashauri hiyo  kuweka mkakati wa kudumu wa kudhibiti msongamano wa malori katika eneo la Mbalizi.

Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Beno Malisa amesema, maegesho holela ya malori yamekuwa yakileta usumbufu kwa watumiaji wa barabara na wakati mwingine kusababisha ajali kutokana na kuziba muonekano wa baadhi ya maeneo muhimu ya barabara.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Erica Yegela, amesema halmashauri imetenga eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari saba katika Bonde la Songwe ambapo stendi hiyo itajengwa.

Amesema stendi hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya malori 80 kwa siku, hatua itakayomaliza changamoto ya maegesho holela katika Mji wa Mbalizi na wakati huo huo kuongeza mapato ya halmashauri kupitia ushuru wa maegesho.

Yegela ameongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya mikakati ya kuboresha usalama wa barabara, kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa usafirishaji wa mizigo ndani ya wilaya hiyo.