
Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule, amesema serikali inapaswa kuzitambua na kushirikiana kwa karibu na kampuni zinazojihusisha na biashara ya ardhi na mali isiyohamishika ili kurahisisha uwekezaji na kuimarisha mipango ya maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Amesema serikali inao wajibu wa kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha huduma zinazohusiana na ardhi, vibali vya ujenzi na umilikishaji wa maeneo zinatolewa kwa wakati ili kuepusha ucheleweshaji unaoweza kusababisha wananchi au wawekezaji kuvunja sheria kutokana na kucheleweshewa huduma.

Senyamule,amesema hayo jijini hapa leo Juni 24,2026 wakati akizungumza kwenye uzinduzi rasmi wa Ofisi na kampuni ya Landmax Real Estate Company Limited hafla iliyosindikizwa na kaulimbiu ya “Tunatimiza ndoto zako za umiliki wa ardhi na makazi bora.”
Senyamule amesema kuwa ardhi ya Dodoma ni utajiri mkubwa unaoendelea kuongezeka thamani kutokana na kasi ya ukuaji wa jiji hilo na ongezeko la watu pamoja na wawekezaji wanaohamia katika Makao Makuu ya Nchi.
Amesema kuwa tofauti na maeneo mengine ambako thamani ya ardhi hubaki ile ile kwa miaka mingi, Dodoma imeendelea kushuhudia ongezeko la haraka la thamani ya ardhi kutokana na mahitaji makubwa ya makazi na uwekezaji.
Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji uliofanywa na Landmax Real Estate Company Limited ni hatua sahihi inayokwenda sambamba na juhudi za maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Hivyo Senyamule amepongeza kampuni hiyo kwa kujenga msingi wa uwaminifu katika utoaji wa huduma zake, akibainisha kuwa sifa hiyo ni muhimu katika kujenga imani kwa wananchi na kupunguza changamoto za utapeli katika sekta ya ardhi.

“Natoa wito kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha zinaendana na kasi ya maendeleo ya wananchi na wawekezaji kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi,”amesema.
Awali, Mkurugenzi wa Landmax Real Estate Company Limited ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi, Onesmo Mnkondya,alisema kampuni hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwaunganisha wananchi na fursa mbalimbali za umiliki wa ardhi, mali isiyohamishika pamoja na uwekezaji.
“Ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya makazi, biashara na jamii kwa ujumla, lakini wananchi wengi bado wanakabiliwa na changamoto za kupata ardhi salama pamoja na huduma sahihi za uwekezaji.
“Hivyo suluhisho ni Landmax inatoa huduma mbalimbali zikiwemo uuzaji na ununuzi wa ardhi na mali isiyohamishika, ushauri wa uwekezaji wa ardhi, usimamizi wa mali, urasimishaji wa nyaraka za ardhi, uendelezaji wa miradi, tafiti za soko na ushirikiano katika miradi ya maendeleo.
Ili kupata huduma hizo aliwakaribisha wananchi kufika Barabara ya Nane,Dodoma Jengo Jipya la CCT, mkabala na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zilipo Ofisi za Landmax Real Estate Company huku akitaja mawasiliano kwa huduma zaidi ambayo ni 0756 800 070.

Hata hivyo hafla hiyo ya uzinduzi ilisindikizwa na, Balozi wa Landmax na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu Baba Levo, ambapo amesema uwepo wa kampuni hiyo utasaidia kupunguza matukio ya wananchi kutapeliwa katika biashara za ardhi na mali isiyohamishika.
Pamoja na hayo ,Balozi huyo aliwataka madalali wa ardhi kushirikiana na kampuni hiyo ili kuhakikisha miamala yote inafanyika kwa uwazi, usalama na uhakiki wa nyaraka, hatua itakayosaidia kupunguza migogoro ya ardhi na vitendo vya utapeli.


More Stories
Serikali kuendelea kupanua fursa elimu Singida
Kumekucha CDF Cup 2026, NMB yaweka Sh milioni 150
TISEZA Songea kuvutia uwekezaji, ajira zaidi zapatikana