Na Joyce Kasiki, Dodoma
SERIKALI imesema inaendelea kuchukua hatua za kuongeza upatikanaji wa elimu ya juu nchini, ikiwemo kupitia ujenzi wa kampasi mpya za vyuo na taasisi za elimu ya juu katika mikoa mbalimbali, huku Mkoa wa Singida ukiwa miongoni mwa maeneo yanayonufaika na jitihada hizo.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wanu Hafidh Ameir wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Mjini, Yagi Kiaratu, aliyeuliza: “Je, lini Serikali itajenga Chuo Kikuu katika Mkoa wa Singida ili kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa eneo hilo?”
Akijibu swali hilo, Wanu alisema Serikali inaendelea kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kupitia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza udahili wa wanafunzi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Serikali inaendelea na ujenzi wa kampasi mpya za vyuo na taasisi za elimu ya juu katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Mkoa wa Singida.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, ujenzi wa kampasi mpya ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) mkoani Singida unaendelea kwa gharama ya dola za Marekani milioni nane, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa umefikia asilimia 61.
Aidha, alisema kwa sasa Mkoa wa Singida unahudumiwa na Kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), ambacho kinatoa fursa kwa wananchi kupata elimu ya juu kupitia mfumo wa elimu huria na masafa.
Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuboresha upatikanaji wa elimu ya juu nchini kulingana na vipaumbele vya maendeleo na uwezo wa rasilimali fedha zilizopo, kwa manufaa ya wananchi wa Singida na maeneo mengine nchini.

More Stories
Senyamule:Serikali inapaswa kuzitambua Kampuni zinazofanya biashara ya ardhi
Kumekucha CDF Cup 2026, NMB yaweka Sh milioni 150
TISEZA Songea kuvutia uwekezaji, ajira zaidi zapatikana