June 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni za Algeria zasaka wabia wa biashara nchini

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Kampuni za Algeria zinazojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za viwandani na kilimo zinatafuta wabia wa kufanya nazo biashara ya mazao na uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini Tanzania.

Kampuni hizo zilizovutiwa kushirikiana na Tanzania zinashiriki katika Maonesho ya 57 ya Biashara ya Kimataifa ya Algiers (FIA) yaliyofunguliwa na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria mnamo Juni 22, 2026, katika Kituo cha Maonesho cha Shirika la Maonesho na Biashara ya Nje la Algeria (SAFEX).

Maonesho haya ndiyo makubwa zaidi miongoni mwa maonesho ya kimataifa nchini Algeria yakiwa yanazishirikisha jumla ya kampuni 731 zinazojumuisha 549 za Algeria kutoka katika kila sekta na kampuni za kigeni 202 kutoka nchi 36 zikiwemo 16 za Afrika.

Akizungumza katika siku ya pili ya maonesho kwenye banda la Tanzania, Balozi Mobhare Matinyi amezitaja kampuni hizo zinazotafuta wabia nchini kuwa ni GISB inayotaka kuuza vifaa vya umeme na kutengeneza nyaya za umeme kwa kutumia shaba ya Tanzania na GETEX inayotaka kununua katani na pamba na kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi.

“Afisa Mtendaji Mkuu wa GISB, Dkt. Mohamed Khelifa, anakuja tena nchini mwezi Julai baada ya ziara yake ya kwanza mwezi Mei 2026 wakati watendaji wakuu wa kampuni tatu tanzu za GETEX wamepanga kuja nchini mwezi Oktoba 2026 kutembelea Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro (KLICL) ili kuona namna ya kushirikiana”, amesema Balozi Matinyi.

Kampuni zingine ni Tapidor inayotengeneza na kuuza mazulia pamoja na nyasi bandia za viwanja vya soka, Optimaflex ya magodoro, Géant Electronics ya bidhaa za umeme, Bellat ya kusindika nyama na ujenzi wa makaazi pamoja na SARL CPC inayotaka kununua dagaa wa baharini na samaki aina ya jodari ambayo Meneja Mkuu wake, Samir Benhamada, ataitembelea Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) mwezi Julai 2026.

Balozi Matinyi ameongeza zaidi kuwa: “Kampuni zingine za Algeria zinataka kununua bidhaa za kahawa, korosho, ndizi, maharage ya soya, mchele, maziwa ya unga na nyama za ng’ombe, mbuzi na kondoo ambazo huliwa kwa wingi nchini Algeria,” akitolea mfano wa sikukuu ya Idi Al-Adha ambapo Serikali ya Algeria iliingiza kondoo milioni moja kutoka nje ya nchi.

Katika maonesho haya Tanzania inatangaza fahari yake ya utalii wa hifadhi, fukwe za bahari, milima, historia ya kale na utamaduni pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta za madini, viwanda, kilimo, nishati na usafirishaji na vilevile mazao ya chakula na biashara.

Mbali ya Ubalozi, taasisi mbili za Serikali ya Tanzania zinazoshiriki ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inayowakilishwa na Meneja wa Tehama na Takwimu, Robert Mtendawema; na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) inayowakilishwa na Kaimu Mhasibu Mkuu Gilbert Lyimo na Afisa Hesabu Mkuu Omary Mafita.