
Na Moses Ng’wat, Ileje.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ileje, Mkoani Songwe, imekabidhi hundi ya Sh milioni 214 kwa vikundi 19 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Hundi hiyo ilikabidhiwa Juni 23, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, katika hafla ya ugawaji mikopo iliyoenda sanjari na kongamano la Jukwaa la Vijana na Wanawake Fursa Forum lililofanyika katika Ukumbi wa RM, Wilayani humo.
Wanufaika wa mikopo hiyo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema itawasaidia kujinasua na mikopo ya “kausha damu” iliyokuwa ikiwabana kwa riba kubwa na masharti magumu.

Walisema kabla ya mpango huo walikuwa wakifanya kazi chini ya mikataba ya pikipiki yenye masharti magumu yaliyowafanya kufanya kazi kwa muda mrefu bila kumiliki mali zao.
Mwenyekiti wa bodaboda stendi ya Itumba, Benisoni Kibona, alisema walikuwa wakilipa takribani Sh 300,000 kwa mwaka kwa waajiri wao hali iliyowafanya kuingiza kipato kikubwa bila kujijengea mali binafsi.
Elisha Mlungu, dereva bodaboda, alisema mikopo hiyo imewapa uhuru wa kufanya kazi bila shinikizo la mikataba kandamizi na kuongeza uwezo wa kipato chao cha kila siku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Nuru Kindamba, alisema mikopo hiyo ni sehemu ya sera ya asilimia 10 inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo baadhi ya vikundi vimepatiwa pikipiki 11 na bajaji 2.

Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri imetoa jumla ya Sh milioni 974 kwa vikundi 116, ikiwa ni mwendelezo wa mpango wa kuinua uchumi wa wananchi wa chini.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, alisisitiza wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili iwe chachu ya maendeleo endelevu kwao na jamii kwa ujumla.


More Stories
Mifumo miwili yazinduliwa kilele wiki ya Utumishi
Kampuni za Algeria zasaka wabia wa biashara nchini
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, yasogeza huduma kwa wananchi