
Na Israel Mwaisaka, Rukwa
Katika jitihada za kuhakikisha fedha za maendeleo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Rukwa imeendesha mafunzo maalumu kwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo kutoka halmashauri zote za mkoa huo, yakilenga kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa miradi.
Akifungua mafunzo hayo jana Juni 23,2026 jijini Sumbawanga, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, amewataka wasimamizi wa miradi kutumia elimu wanayopewa kama nyenzo ya kuimarisha usimamizi wa miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Nyerere amesema utekelezaji wa miradi bila kuzingatia sheria, kanuni za manunuzi na taratibu za ujenzi unaweza kusababisha migogoro, hasara kwa Serikali na kuchelewesha huduma muhimu zinazotarajiwa na wananchi.
“Miradi ya maendeleo ni matumaini ya wananchi. Ni wajibu wa kila msimamizi kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa uadilifu na miradi inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa na kwa wakati,” amesema.
Kwa upande wake, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa, Mzalendo Widege, amesema mafunzo hayo yanalenga kujenga uelewa wa pamoja kati ya wasimamizi na wafuatiliaji wa miradi ili kuzuia mianya ya ubadhirifu, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha miradi inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Amesema usimamizi bora wa miradi ni msingi wa maendeleo endelevu, kwani uongeza thamani ya fedha za umma na kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali.
Kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Missana Kwangura, ameishukuru TAKUKURU kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo amesema yamewapa maarifa muhimu yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Kwangura amesema washiriki wamejipatia uelewa mpana kuhusu wajibu wao katika kusimamia rasilimali za umma na kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata kwa kuzingatia sheria, kanuni ,miongozo na taratibu zote za usimamizi wa miradi.
Mpango huo wa TAKUKURU unatarajiwa kusaidia kupunguza malalamiko yanayohusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuimarisha uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma na kuhakikisha kila shilingi ya maendeleo inaleta matokeo chanya kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa.



More Stories
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, yasogeza huduma kwa wananchi
Mil.214 zawanasua na mikopo ‘Kausha damu’ Ileje
Watumishi wa Umma wakumbushwa matumizi ya “PEPMIS”