June 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washindi ‘kila muamala bao la ushindi’ waendelea kupeta

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya huduma za fedha kidigitali, Mixx imeendelea kuhimiza matumizi ya malipo ya kidijitali nchini, ikiwataka wafanyabiashara kutumia suluhisho za kisasa kama Lipa Namba ili kuongeza ufanisi, usalama na urahisi katika shughuli zao za kila siku.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa droo ya nne ya kampeni ya “Kila Muamala ni Bao la Ushindi”, inayofanywa na Mixx kwa kushirikiana na kampuni ya Hisense.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mixx, Arnold Ngarashi, amesema matumizi ya malipo kidijitali yanaendelea kubadilisha namna biashara zinavyoendeshwa kwa kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na kuongeza usalama wa miamala.

Amesem, huduma kama Lipa Namba zinawapa wafanyabiashara njia rahisi na salama ya kupokea malipo, huku pia zikisaidia kupunguza changamoto ya kutoa chenji na kuboresha usimamizi wa fedha za biashara.

Kwa mujibu wa Ngarashi, ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali linaashiria mabadiliko ya mtazamo miongoni mwa wafanyabiashara na wananchi kuelekea matumizi ya huduma za kifedha za kisasa na jumuishi.

Ameogeza kuwa, Mixx itaendelea kuwekeza katika suluhisho bunifu za kifedha ili kurahisisha miamala na kusaidia ukuaji wa biashara nchini.

Akizungumzia kampeni ya “Kila Muamala ni Bao la Ushindi”, amesema zaidi ya Watanzania 30 tayari wamejishindia zawadi za fedha taslimu zenye thamani ya shilingi milioni moja kila mmoja tangu kuanza kwa kampeni hiyo.

Amesema, kampeni hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha kidijitali kwa kuwazawadia wateja wanaofanya miamala kupitia jukwaa la Mixx, huku zawadi kuu ikiwa ni shilingi milioni 50.

Mmoja ya washindi waliokabidhiwa zawadi zao, James Mlugangala amesema huduma za Mixx zimemrahisishia kufanya miamala kwa haraka na usalama, na kwamba fedha alizoshinda zitasaidia kukuza biashara yake pamoja na kutekeleza mipango mingine ya maendeleo.

Kampeni ya “Kila Muamala ni Bao la Ushindi”, inayofanyika kwa ushirikiano na Hisense chini ya kaulimbiu ya “Ikiingia Tu Goli”, ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha kidijitali nchini na kushiriki furaha ya Kombe la Dunia na watanzania.

Kupitia kampeni hiyo na huduma zake, Mixx inalenga kuchangia juhudi za kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali miongoni mwa Watanzania.