Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Kilolo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza utekelezwaji wa mradi wa Chuo cha elimu ya ufundi stadi (VETA) Kilolo utakao gharimu zaidi ya Sh Bil1.6 hadi kukamilika kwake.
Mradi huo utakapokamilika utakuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya elimu ya ufundi inayotekelezwa katika Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kujiajiri.
Hayo yameelezwa leo Juni 19, 2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapjnduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, wakati wa ziara yake alipofika na kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo.

Amesema, vijana na wananchi wa Wilaya ya Kilolo wanatarajia kunufaika na mradi huo wa Ujenzi wa Chuo cha elimu na ufundi stadi (VETA) unaoendelea katika Kijiji cha Luhindo, Kata ya Mtitu, ambao unatarajiwa kutoa mafunzo ya ufundi stadi, kuongeza ajira na kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi mara baada ya kukamilika kwake.
Katika ziara hiyo, Kihongosi amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wanailinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kihongosi amesisitiza kuwa elimu ya ufundi ni miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo ya Taifa kwani huwapa vijana maarifa na stadi zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na ujenzi wa uchumi.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyowasilishwa na Afisa Mthibiti Ubora wa Shule Wilaya ya Kilolo, Alto Kinunda, chuo hicho kinajengwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari 38.16 na utekelezaji wake unafanyika kwa awamu mbili.

Kinunda amesema awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa majengo tisa ambayo ni jengo la utawala, madarasa, vyoo vya jumuiya, karakana ya umeme na mabomba, karakana ya uashi na useremala, karakana ya upishi na ushonaji, nyumba ya mtumishi, jengo la mlinzi pamoja na jengo la umeme.
“Na hadi sasa maendeleo ya mradi yamefikia asilimia 76 huku baadhi ya majengo yakiwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji ikiwemo uwekaji wa vifaa vya umeme, maji, rangi na mifumo ya maji taka.”amesema Kinunda huku akiongeza kuwa
“Mpaka sasa mradi umepokea zaidi ya Sh. Mil 777 na hakuna mzabuni anayetudai na kazi zinaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri,”
Kinunda amefafanua kuwa awamu ya pili ya mradi itahusisha ujenzi wa karakana ya ufundi magari, karakana ya uungaji vyuma, jiko, ukumbi wa chakula, maktaba, mabweni, stoo pamoja na nyumba za wakufunzi.
Aidha, Kinunda amesema ubora wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo unadhibitiwa kwa kufuata viwango vinavyotakiwa, huku vifaa kama saruji, nondo, kokoto, mchanga na tofali vikifanyiwa ukaguzi na taasisi husika kabla ya kutumika.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Ritta Kabati, amesema uwepo wa chuo hicho ni hatua muhimu katika kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuondokana na utegemezi wa ajira za kuajiriwa.
“Mradi huu ni uwekezaji mkubwa kwa vijana wetu. Tunatarajia kuona wahitimu wengi wakipata ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na hata kuajiri wengine katika jamii,” amesema Kabati.
Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili, wananchi waliohudhuria ziara hiyo wameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo, wakisema utachangia kuongeza ajira kwa mafundi, vibarua, mama lishe, waendesha bodaboda na watoa huduma mbalimbali katika eneo hilo.
Mmoja wa wananchi katika eneo Mtitu, Maria Stambuli amesema kukamilika kwa chuo hicho kutawapa vijana wa Kilolo fursa ya kupata mafunzo karibu na makazi yao badala ya kusafiri kwenda maeneo ya mbali kutafuta elimu ya ufundi.

“Chuo hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa vijana wetu na wengi watapata ujuzi na kuanzisha shughuli za kujipatia kipato jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira,” amesema Stambuli.
ok

More Stories
PPAA yajivunia mafanikio Moduli ya Malalamiko,Rufaa
Serikali yahimiza wazazi maleI ya watoto
Serikali yakiri Shule iliyojengwa na NMB ina viwango