
Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
ZAIDI ya Taasisi 14,000 zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi nchini zimekamilisha usajili wao kwa hiari katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), hatua iliyoelezwa kuwa ni mwitikio chanya wa wadau katika kuimarisha ulinzi wa faragha na usalama wa taarifa za wananchi.
Hata hivyo, PDPC imeonya kuwa taasisi zote zinazoendelea kukusanya au kuchakata taarifa binafsi bila kusajiliwa zinatenda kosa la kisheria na zinakabiliwa na hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo faini na adhabu za kiutawala kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.
Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema utekelezaji kamili wa sheria hiyo ulianza Aprili 9, 2026 mara baada ya kufungwa kwa kipindi cha usajili wa hiari kilichomalizika Aprili 8, 2026.
Dkt. Mkilia amesema usajili wa taasisi hizo unaonesha dhamira ya wadau katika kuhakikisha taarifa binafsi za wananchi zinalindwa kwa mujibu wa sheria na viwango vinavyotakiwa katika mazingira ya huduma za kidijitali.
Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, ni marufuku kwa taasisi yoyote kukusanya au kuchakata taarifa binafsi bila kusajiliwa na Tume kama mkusanyaji au mchakataji wa taarifa hizo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa sheria hautakuwa na msamaha kwa watakaokiuka matakwa yaliyowekwa.
Aidha, ameeleza kuwa bado kuna baadhi ya taasisi, hususan katika sekta za afya na elimu, zinazoendelea kufanya shughuli hizo bila kuzingatia sheria, jambo ambalo linaweza kuhatarisha haki za msingi za wananchi kuhusu faragha na usalama wa taarifa zao.
Kutokana na hali hiyo, aliagiza taasisi zilizoanza mchakato wa usajili lakini hazijaukamilisha kufanya hivyo ndani ya siku saba za kazi kuanzia Juni 12, 2026, huku taasisi ambazo hazijaanza kabisa usajili zikielekezwa kuanza na kukamilisha mchakato huo ndani ya muda huo.
Wakati huo huo, Dkt. Mkilia amesema PDPC inatarajia kuandaa Kongamano la Kwanza la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuanzia Juni 29 hadi Julai 1, 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kwa lengo la kuwakutanisha wataalamu na wadau mbalimbali kujadili maendeleo ya teknolojia na kuimarisha usalama wa huduma za kidijitali nchini.

More Stories
Senyamule:Serikali inapaswa kuzitambua Kampuni zinazofanya biashara ya ardhi
Serikali kuendelea kupanua fursa elimu Singida
Kumekucha CDF Cup 2026, NMB yaweka Sh milioni 150