June 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM waibuka kidedea Udiwani kata ya Kala

Na Israel Mwaisaka, Nkasi

‎Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa Udiwani kata ya Kala wilayani Nkasi baada ya John Japheth Sikazwe kupata kura 7625  za ndiyo kati ya kura 7705 zilizopigwa .

‎Kwa mujibu wa George Mwahinda Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Nkasi kusini na Nkasi kaskazini ni kuwa waliojiandikisha kupiga kura ni 8832,Waliopiga kura 8,079,kura halali 8037, na kura zilizoharibika 53

‎Amesema kuwa uchaguzi huo ambao ilikua na mgombea mmoja wa CCM John Japheth Sikazwe ilikua ni kupigiwa kura za ndiyo au hapana,hivyo mgombea huyo alikubalika kwa kupigiwa kura 7625 na za hapana ilikua 70 sawa na asilimia 99.1 ya kura zote zilizopigwa.

‎Kufuatia matokeo hayo kwa mujibu wa kifungu Cha 106 Cha Sheria ya uchaguzi Urais,Ubunge na Udiwani  John Sikazwe alitangazwa rasmi kuwa mshindi wa nafasi hiyo ya Udiwani katika kata hiyo ya Kala

‎Katibu wa CCM Wilaya Nkasi Anastazia Almas kwa upande wake amewashukuru Wananchi wa kata hiyo kwa kuendelea kukiamini chama hicho kwani hata Diwani aliyekuwepo awali alitokana na chama hicho.

‎Na alidai kuwa kuchaguliwa ni hatua moja lakini kuwatumikia Wananchi ni jambo lingine hivyo kwa Imani hiyo iliyoonyeshwa na Wananchi Diwani huyo ni lazima awajibike ipasavyo  kwa kuwatumikia Wananchi.

‎Amedai kuwa kata hiyo bado ina changamoto nyingi hasa katika sekta ya elimu na miundo mbinu hivyo Diwani huyo analo jukumu la kuikumbusha Serikali juu ya changamoto hizo ili kuwapatia ahueni Wananchi.