May 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mke adaiwa kumuua Mumewe kwa sindano yenye sumu

Na Moses Ng’wat, Mbozi.

Queen Mbuba, Mkazi wa Kijiji cha Igunda, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe, anadaiwa kumuua mume wake baada ya kumchoma sindano inayodaiwa kuwa na sumu na baadaye kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali.

Taarifa iliyotolewa Mei 26, 2026 kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, imeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Mei 22 mwaka huu majira ya saa 9:00 alasiri kijijini hapo, huku marehemu akitambulika kwa jina la Shizya Mwangwale (35).

Kwa mujibu wa Kamanda Senga, baada ya tukio hilo mwanaume huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kwa matibabu, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kutokana na hali yake kuwa mbaya zaidi.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alichomwa sindano begani kushoto inayodhaniwa kuwa na sumu, kabla ya kushambuliwa kwa kitu chenye ncha kali tumboni upande wa kulia.

Imeelezwa kuwa baada ya kuchomwa sindano hiyo, Shizya alimuuliza mtuhumiwa kuhusu kilichokuwa kimewekwa mwilini mwake kupitia sindano aliyochomwa, ndipo mtuhumiwa alidai kuwa ilikuwa ni dawa ya kutibu tatizo la miguu lililokuwa likimsumbua.

Kamanda Senga amesema chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na wivu wa kimapenzi, ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mumewe (marehemu) kuwa na mahusiano na wanawake wengine.

Ameongeza kuwa mara baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alitoweka na Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali wa kumtafuta ili aweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo, huku likisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia njia za kisheria na usuluhishi katika kutatua migogoro ya kifamilia na kijamii badala ya kujichukulia sheria mkononi.