May 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIDA yasajili zaidi ya watu mil.1.1 miezi 10

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi  amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeendelea kuimarisha huduma za usajili na utambuzi wa wananchi, ambapo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026 jumla ya watu 1,145,334 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wamesajiliwa na kutambuliwa.

Amesema hayo jijini hapa leo Mei 25,2026 bungeni jijini hapa wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2026/27 ambapo amesema idadi hiyo ni ongezeko ikilinganishwa na watu 844,994 waliosajiliwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Waziri Katambi amesema hatua hiyo imefanya jumla ya watu waliosajiliwa na kutambuliwa nchini kufikia 27,186,421.

Aidha, amesema NIDA imetoa Namba za Utambulisho wa Taifa kwa watu 857,244 katika kipindi hicho, hatua iliyofikisha jumla ya wananchi waliopata Namba za Utambulisho wa Taifa kufikia 22,654,206.

“Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya usajili na utambuzi ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hizi muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,”amesema Bashungwa.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema  taasisi 17 zimeunganishwa kwenye Mfumo wa Usajili na Utambuzi katika kipindi hicho, na hivyo kufanya jumla ya taasisi zilizounganishwa kufikia 147.

Ameeleza kuwa kuunganishwa kwa taasisi hizo kunasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Serikali na binafsi, sambamba na kuimarisha usalama wa taarifa za wananchi.